Chifu (Mwene) Nzunda kiongozi mkuu wa Wanyiha
HISTORIA.
Wanyiha ni kabila ambalo linapatikana katika wilaya ya Mbozi na linachukua robo tatu (75%) ya wakazi wa wilaya ya Mbozi. Mbali na Wanyiha, Mbozi ina makabila mengine ambayo huchukua robo (25%) ya wakazi wote. Makabila hayo ni Wandali kutoka wilaya jirani ya Ileje, Wamalila na Wasafwa kutoka wilaya ya Mbeya, Wanyakyusa kutoka wilaya za Rungwe na Kyela, Wabungu kutoka Wilaya ya Chunya na Wasangu kutoka Mbarali. Makabila mengine yanayopatikana Mbozi ni Wakinga, Wahehe, Wabena, Wafipa, Wangoni na mengineyo mengi.
Historia inaonyesha hapo zamani Wanyiha walikuwa na machifu wakubwa watatu tu ambao walikuwa na wasaidizi wao. Machifu hao walikuwa ni Mwene Nzunda, Mwene Mwamlima na Mwene Nzowa. Kwa kuwa maeneo ya kiutawala yalikuwa makubwa, wasaidizi wa machifu walitumika kama watawala wadogo. Wasaidizi hao walijulikana kwa Kinyiha ‘Abhahombe’. Kazi hii haikuwa na mshahara wowote japo kulikuwa na eneo kubwa la kutawala wakaamua kuwatawaza wasaidizi wao kuwa machifu ili kurahisisha kazi za kiutawala. Hadi sasa zaidi ya koo 20 ambazo awali zilikuwa zinasaidia shughuli za kichifu za kinyiha sasa ni koo za kichifu.
UTATUZI WA MIGOGORO
Kwa Wanyiha walikuwa na mbinu mbalimbali za kutatua migogoro yao. Mbinu kubwa iliyokuwa ikitumiwa na wazee kutatua migogoro ilikuwa ni vikao ambavyo viliitishwa mara tu wanapoona kuna jambo liko kinyume na mila au maadili katika jamii. Vikao hivyo viliweza hata kutoa adhabu kwa mtu aliyebainika kuwa mkorofi na kufanya wengine waogope kufanya mambo yanayokatazwa na wazee. Baadhi ya adhabu zilizotolewa ni kuchapwa viboko hadharani, kununua pombe, kulipa fedha na kulipa mbuzi.
Vikao hivyo vilitegemea sana mkosaji anavyokubali au kukataa kosa Mfano walikuwa wanatuma mtu kumwita Yule aliyekosa kuhudhuria kikao , kabla ya kwenda alikuwa naye anamrudishia majibu Yule aliye mletea ujumbe kuhusu kumuomba radhi kwa wazee wa mila.Hali hiyo ilikuwa inapunguza hasira kwa wazee hivyo hata adhabu haikuwa kali kama yule aliyeleta jeuri.
Njia hii ndio iliyowawezesha kutatua migogoro yote ikiwa ni ile ya ndoa, mtu kushikwa ugoni, Ardhi, uharifu wa Mazingira.Pia ikumbukwe na kuwqa kosa linapofanywa na mtu lilichukuliwa kama kosa la ukoo mzima hivyo lilifanya ukoo kuonyana wao kwa wao hata kabla kuitwa na wazee wa mila.
Kulingana na mwingiliano wa sasa na watu kudharau mila, nguvu ya wazee wa mila ya kutatua migogoro yao wenyewe na kutoa adhabu imepotea na kuwafanya pale wanapopata tatizo na kushughulikia bila kufikia muafaka kuirushia serikali ili kumaliza kwa njia ya mahakama au vyombo vingine vya kisheria.
HIFADHI YA MAZINGIRA
Wanyiha huamini kuwa maeneo ambayo yana chemichemi huwa yana nyoka mkubwa ambaye ndiye anayesaidia upatikanaji wa maji hayo na kuwa ukimuua nyoka huyo eneo hilo halitakuwa na maji tena. Kutokana na imani hiyo eneo hilo lilichukuliwa katika uangalizi mkubwa na hakuna mtu aliyeruhusiwa kukata miti au kuua nyoka yoyote aliyeonekana eneo hilo na kufanya vyanzo vya maji kulindwa na hivyo kuwa katika hali ya usalama ukilinganisha na hali ya sasa.
Si hivyo tu, kabila hili linaamini sana mizimu na watu wenye mizimu hujengewa imani sana kuwa ni watu wenye uono na hutoa msaada kwa jamii pale mtu anapoonewa hususani kwa njia ya ushirikina kwa kutoa dawa ambazo hutokana na miti. Shughuli za watu wenye mizimu hufanyika porini kutokana na kuwa na imani hiyo wanaamini kuharibu misitu kutafanya watu wenye mizimu kushindwa kutatua matatizo yao kwani dawa hazitapatikana.
Ukataji wa miti aina ya mibula haukuruhusiwa kabisa kwani miti hiyo iliaminika kuwa na utabiri wa kujua kama ni mwaka wa njaa au la. Mibula ikizaa sana matunda wazee walichukulia kuwa mwaka huo ni mwaka wa njaa na matunda hayo yalikuwa yakitumika kama chakula wakati wa njaa pia walitumia juisi iliyotokana na mibula kwa ajili ya kuweka kwenye uji kama sukari.
SHUGHULI ZA KIUCHUMI.
Wanyiha walijishughulisha na shughuli mbalimbali ikiwa ni pamoja na kilimo, ufugaji na uhunzi. Katika kilimo walilima mazao kama ulezi ambalo lilikuwa zao la chakula, walilima maharage na baadaye baada ya kuletwa mazao mengine kama mahindi, karanga, kahawa waliendelea kulima. Pia walikuwa wanafuga wanyama kama vile mbuzi, ng’ombe, punda, kuku.
Baadhi ya wengine walijishughulisha na kazi ya uhunzi ambao ndio waliokuwa wanatengeneza zana mbalimbali zilizokuwa zinatumika kwa ajili ya shughuli za kilimo. Zana zilizotengenezwa zilikuwa ni mishale, mikuki, shoka, visu na majembe. Ufundi huu umeendelea hadi leo wapo watu katika kabila hili la Wanyiha wanaoshughulika na uhunzi kama kazi inayowapatia kipato
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.