FOLENI YA MALORI TUNDUMA, RC MICHAEL AUNDA TIMU YA UTATUZI.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Dkt. Francis Michael ameunda timu maalumu ambayo itakuwa na kazi ya kutatua foleni ya Malori iliyopo katika Mji wa Tunduma, timu hiyo ni kutoka kwa madereva ambao watawakilishwa na vyama vyao, TANROADS, TRA, Jeshi la Polisi (RTO) na mawakala.
Mkuu wa Mkoa ameunda timu hiyo baada ya kufanyika kikao kazi cha utatauzi wa foleni ya Malori kilichowakutanisha viongozi kutoka vyama vya madereva, wamiliki wa Malori, Mawakala wanaovusha magari, Mamlaka ya mapato Tanzania (TRA), Wakala wa Barabara (TANROADS) Songwe, Jeshi la Polisi pamoja na viongozi kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya ya Momba kilichofanyika ofisini kwake, Juni 14.
Mkuu wa Mkoa amesema timu aliyoiunda inatakiwa kuwasilisha mapendekezo, maoni ya muda mfupi na ya muda mrefu kuhusu utatauzi wa foleni ya Malori kwa kuwa wao ndio wanazijua changamoto vizuri.
"Kuna changamoto ambazo ziko ndani ya uwezo wetu hapa, hivyo nendeni mfanye kazi kwa pamoja na mje na majibu sahihi ya nini tufanye Serikali kwa kushirikiana na nyinyi katika kutatua foleni hii" Mhe. Dkt. Francis Michael.
Mkuu wa Mkoa, Mhe. Dkt. Francis Michael ameielekeza timu hiyo kufanya kazi kwa wazi, bila upendeleo katika kutatua foleni iliyopo Mji wa Tunduma.
Wakati timu iliyoundwa inaendelea kufanya kazi yake, Mkuu wa Mkoa, Mhe. Dkt. Francis Michael ameendelea kufanya mazungumzo ya kidplomasia na viongozi wa Serikali ya Zambia kutoka Mkoa wa Muchinga kutatua mambo yaliyopo ndani ya uwezo wa viongozi hao.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.