JITIHADA ZAIDI ZINAHITAJIKA KUONGEZA UFAULU KIDATO CHA SITA.SONGWE:
Waratibu elimu kata amewatakiwa kuongeza jitihada zaidi katika usimamizi wa shule ili kuongeza ufaulu wa wanafunzi wa kidato cha sita.
Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Tawala Mkoa, Ndg. Steven Pankras wakati akifungua kikao kazi cha waratibu elimu Kata, Maafisa elimu, wathibiti ubora wa Shule, pamoja na tume ya utumishi wa waalimu kilichofanyika Julai 8 ukumbi wa ofisi ya Mkuu wa Mkoa.
Ndg. Pankras amesema licha ya waalimu kujitahidi kuondoa daraja la sifuri kwa kidato cha sita lakini bado mkoa haujafanya vizuri ukilinganisha na idadi ya wanafunzi waliopo kwa kidato cha sita.
"Miaka ya nyuma miundombinu ndio ilikuwa kikwazo kwa wanafunzi kufaulu lakini saizi Serikali ya awamu ya sita imejitahidi kuboresha miundombinu ya shuleni hivyo kazi imebaki kwetu waalimu, tuongoze bidii kwa hili" amesema Pankras.
Mwaka huu Wanafunzi wapatao 1,353 katika shule 18 wamefanya mtihani wa kuhitimi kidato cha sita katika matokeo Yao waliopata daraja la kwanza walikuwa 351, daraja la pili 773, daraja la tatu 205 na daraja la nne ni 1 huku daraja la sifuri hakuna wanafunzi aliyepata.
"Unakuta shule ina wanafunzi 12 au 7 lakini inashindwa kutoa daraja la kwanza kwa wanafunzi wote hii haijakaa vizuri kabisa" amesema Pankras.
Aidha, Ndg. Pankras amesema lengo la Mkoa wa Songwe ni kuona shule zinafanya vizuri kwa kuongeza daraja la kwanza na la pili, amewataka viongozi wa elimu kuanzia ngazi ya Kata hadi Mkoa kutofurahia kuondoa daraja sifuri tu bali waongeze kasi ya kuapata daraja la pili na la kwanza ili wanafunzi wapate fursa ya kujiunga na vyuo vikuu mbalimbali.
Afisa Elimu Mkoa wa Songwe, Mwl. Michael Ligola amesema lengo la kikao hicho ni kujadili matokeo ya mtihani wa upimaji wa Kanda wa darasa la saba, kutoa mrejesho wa kikao cha maafisa elimu wa Mkoa kilichofanyika mkoani Tabora na kuweka mikakati bora ya kuongeza ufaulu wa elimu kuanzia msingi hadi kidato cha sita pamoja na kuboresha usimamizi wa miradi.
Afisa elimu msingi Halmashauri ya Mji Tunduma, Mwl. Wilson Mtafya akiongea kwa niaba ya wajumbe wa kikao hicho amesema watakwenda kufanyia kazi mapungufu yote yaliyojitokeza ili kuongeza ufaulu kwani kitendo cha mwanafunzi kushindwa kufanya vizuri kidato cha sita kunapelekea malengo yake kutotimia ya kwenda vyuo mbalimbali.
Ndg. Pankras amezitaka Shule binafsi ziwe chachu ya kuongeza daraja la kwanza kwa kuwa wazazi/walezi wanatoa ada na shule nyingi zina idadi ndogo ya wanafunzi ukilinganisha na za Serikali hivyo tunatarajia makubwa kutoka kwao wakati na za Serikali nazo zinategemewa zifanye makubwa ndani ya Mkoa.
Wakati huo huo, Ndg. Stephen Pankras ametoa wito kwa waalimu kuwajengea uwezo wa kipekee kwa watoto ambao hawajui kusoma, Kuandika na Kuhesabu ili kusitokee mtoto anafika darasa la saba au la nne hajui kusoma, Kuandika na Kuhesabu.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.