Katibu Tawala Mkoa wa Songwe David Kafulila ameahidi huwashughulikia watumishi wanaotoa takwimu za uongo kwakuwa zimekuwa zikikwamisha mipango mbalimbali ya maendeleo.
Kafulila ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya awali ya mipango na bajeti ya masuala ya lishe ngazi ya mkoa na halmashauri yaliyofanyika katika ukumbi wa halmashauri ya Wilaya ya Mbozi mapema wiki hii.
“Watendaji wa halmashauri mmekuwa mkitoa takwimu ambazo sio sahihi jambo ambalo linaathiri mipango mbalimbali, Sitaweza kusita kumchukulia hatua mtumishi yeyote ambaye atafanya makosa hayo na ninaelekeza watendaji ngazi ya mkoa msipokee tu taarifa bila ya kuzihakiki”, amesisitiza.
Aidha Kafulila amewashukuru wadau wa maendeleo akitoa mfano wa shirika la UNICEF ambalo limekuwa likisaidia masuala ya Afya na Lishe na kuongeza kuwa juhudi za wadau hawa hazitafanikiwa endapo takwimu watakazopewa zitakuwa sio sahihi.
Amezielekeza halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya shughuli za lishe kama miongozo inavyosema na kutoa fedha zikatekeleze mipango iliyowekwa huku akimtaka afisa anayesimamia bajeti ngazi ya Mkoa kusimamia utekelezaji wa maelekezo hayo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa Dkt Kheri Kagya amesema wastani wa watoto 37 kati ya 100 mkoani Songwe wamedumaa ikiwa ni kiwango kikubwa kuliko wastani wa kitaifa wa watoto 34 kati ya 100.
Dkt Kagya ameongeza kwa kuwashukuru UNICEF wanaofadhili utafiti wa hali ya lishe kwa mkoa wa Songwe, utafiti ulioanza Septemba 2018 na unatarajiwa kukamilika Januari 2019.
Amesema matokeo ya awali ya utafiti huo bado yanaonyesha kuwa hali ya udumavu Mkoani Songwe si nzuri hivyo halmashauri zifuate maelekezo ya Katibu Tawala Mkoa ya kutenga na kutoa fedha kwa ajili ya masuala ya lishe.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.