Songwe, 07 Novemba 2024 ,
Bi. Happiness Seneda, Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, amefungua rasmi kikao cha tathmini ya huduma za afya ya uzazi na mtoto mkoani Songwe, kikao hicho kitafanyika kwa muda wa siku mbili kuanzia tarehe 07 hadi 08 Novemba, 2024 katika ukumbi wa Hanimuni uliopo Halmashauri ya Mji Tunduma na kimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa afya ngazi ya mkoa, wilaya, na Halmashauri, pamoja na wadau wa sekta ya afya ikiwemo THPS, Amref na Marie Stopes Tanzania.
Bi. Seneda, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuimarisha huduma za afya nchini hususan kwa akina mama na watoto. Amesema lengo la kikao hicho ni kufanya tathmini ya mafanikio na changamoto katika huduma za afya ya uzazi na mtoto, na kujadili mbinu za kukabiliana na vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na vifo vya watoto wachanga mkoani humo. Alieleza kuwa ajenda hiyo ni moja ya vipaumbele vya serikali, ikiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, ambaye ameonyesha dhamira ya dhati katika kupunguza vifo hivyo."
|
Bi. Seneda ameeleza kuwa serikali kupitia Wizara ya Afya na OR-TAMISEMI kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo imeimarisha huduma za afya kwa kuongeza vituo vinavyotoa huduma za uzazi na dharura ya upasuaji. Amebainisha kuwa Mkoa wa Songwe sasa una vituo 18 vyenye uwezo wa kutoa huduma za upasuaji, ikiwa ni pamoja na hospitali za halmashauri na vituo vya afya vilivyopo katika wilaya mbalimbali za mkoa huu.
Vile vile "Mkoa wa Songwe umepata mafanikio makubwa katika kupunguza idadi ya vifo vya uzazi na vya watoto wachanga. Mwaka 2022, kulikuwa na vifo 38 vya akinamama na vifo 320 vya watoto wachanga. Idadi hii ilipungua hadi vifo 33 vya uzazi na 196 vya watoto wachanga mwaka 2023. Aidha, alieleza kuwa bado kuna changamoto kwani hadi Oktoba 2024, vifo 27 vya uzazi vimeshuhudiwa katika mkoa, ambapo sababu kuu zilikuwa ni matatizo ya kutokwa damu nyingi, kifafa cha mimba, na uambukizo."
Aidha ametoa wito kwa watendaji wa afya kuimarisha uhamasishaji kwa wananchi ili kuokoa maisha ya akina mama na watoto wachanga kwa kuwahimiza kwenda kwenye vituo vya afya kwa matibabu ya haraka. Alisisitiza kuwa tatizo la vifo hivyo linaweza kuzuilika kwa usimamizi madhubuti na ufuatiliaji wa huduma zinazotolewa.
Sambamba na hayo, Bi. Seneda ametoa pongezi kwa jitihada za serikali za kuimarisha huduma za rufaa, ambapo Hospitali ya Rufaa ya Mkoa imepata vifaa tiba vya kisasa ikiwemo mashine ya CT-scan na huduma za kibingwa kama magonjwa ya uzazi na watoto, huduma za dharura, pamoja na huduma za mionzi. Uwekezaji huu umesaidia kupunguza rufaa za wagonjwa kwenda hospitali za kanda. Pia amewashukuru wadau wote kwa kuunga mkono jitihada za serikali katika kuboresha huduma za afya mkoani Songwe.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.