Serikali Mkoani Songwe imedhamiria kutangaza fursa za uwekezaji katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii kupitia maadhimisho ya siku ya Kimondo Duniani Juni, 30 yatakayofanyika kwa mara ya kwanza nchini.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa amesema maadhimisho haya yatakayofanyika katika eneo kilipo kimondo cha Mbozi na matarajio ni kuwa yatavutia watalii na wawekezaji kutoka ndani na Nje ya nchi.
Ameongeza kuwa Mkoa wa Songwe unazo fursa za uwekezaji katika utalii, viwanda, kilimo, madini na biashara hivyo wawekezaji wazawa na hata wale wa nje ya nchi wanakaribishwa kuwekeza.
“Maadhimisho haya yatafanyika kwa muda wa siku tatu, tarehe 28 Juni tutakuwa na fainali za mpira wa pete na miguu, tarehe 29 Juni tutakuwa na kongamano la kitaaluma na uwekezaji na tarehe 30 Juni ndio kilele cha maadhimisho ya siku ya kimondo Dunia, tutatoa zawadi kwa washindi mbalimbali na tunarajia kuwa na watu zaidi ya elfu hamsini,” amesema Gallawa.
Aidha Kila halmashauri mkoani Songwe imepewa eneo katika kijiji cha Ndolezi kilipo Kimondo kwa ajili ya kutangaza fursa za uwekezaji, huduma na bidhaa wanazozalisha pamoja na taasisi na Wizara ya Maliasili na Utalii watakuwa na eneo la kutangaza fursa za uwekezaji na utalii nchini.
Gallawa ameongeza kuwa Mkoa wa Songwe unayo maeneo mengi ya utalii ikiwemo eneo lenye majimoto katika Kijiji cha Nanyara, unyayo wa Binadamu wa kale, hifadhi ya wanyamapori ya Piti/Lukwati na maporomoko ya maji.
Kimondo cha Mbozi chenye uzito wa tani 16 ni cha kwanza kwa ukubwa nchini Tanzania, cha pili Afrika na cha nane kwa ukubwa duniani kikiwa na sifa ya pekee ya kuwa na madini ya chuma kwa asilimia 90 hivyo kuwa cha baridi muda wote hata wakati wa jua kali.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.