Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Chiku Gallawa alifanya kikao cha majumuisho baada ya ziara ya kikazi katika Halmashuri ya Mji wa Tunduma ambapo alitaka kujua hatua za utekelezaji wa mkakati wa Taifa kufikia uchumi wa kati na Tanzania ya viwanda ifikapo 2027.
Aidha katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa alisomewa taarifa za utekelezaji wa shughuli za maendeleo ya Kata, alisikiliza kero za Wananchi na kutoa majibu ya papo kwa papo kutoka kwa Wakuu wa Idara na Vitengo, pia alitembelea baadhi ya miradi ili kujiridha na utekelezaji wake.
Katika majumuisho kikao cha majumuisho hayo Mkuu wa Mkoa alianza kwa kuwaeleza Viongozi kuwa “ Kila mmoja wetu hapa, akiwa Mtumishi, kiongozi mwajiriwa, Kiongozi mteuliwa, hajajitambua kuwa anatakiwa kuwahudumia wanyonge wa kipato au kwa kuonewa tu anatakiwa abadilike kwa sababu huko nyuma serikali yetu ilirithi tabia ya Serikali ya Kikoloni ambapo mtumishi alikuwa karibu na Mkoloni na alijiona yuko juu naye ni Bwana wa Wananchi badala ya kuwatumikia. kuanzia sasa tubadilike hata kwenye mikutano Wananchi wasikae juani wakati viongozi wapo kivulini. Uwepo wetu ni kwa ajili ya Wanyonge wa umaskini wa kipato na wengine kwa kuonewa tu, inatakiwa kuwatumikia na kwa ujirani, tutoke maofisini. Na hii ikibadilika kifikra utajituma kweli kumtoa mwananchi kwenye umaskini” alisisitiza.
Baada ya utangulizi huo Mkuu wa Mkoa alitoa maelekezo ambayo alitaka yaanze kutekelezwa mara baada ya kikao hicho kama ifuatavyo:-
Kuwa Watumishi waache kufanya kazi kwa mazoea bali wawe na malengo na wapimwe kwa malengo waliyojiwekea, Wananchi wapewe taarifa ili kushiriki vikao vya Baraza la Madiwani la Halmashauri pia wasomewe mapato na matumizi katika ngazi ya Mtaa, Watendaji wasimamiwe na waweke siku maalum ya kusikiliza kero za Wananchi, Wakuu wa Idara watoke maofisini waende kuwasikiliza wananchi katika maeneo yao, Wananchi washirikishwe moja kwa moja katika kupanga mipango na kutekeleza miradi ya maendeleo kwa sababu miradi ni ya kwao na siyo ya viongozi, Kila pesa zinazoingia katika Halmashauri ziwekwe kwenye mbao za matangazo zikionesha matutumizi yake ili Wananchi waweze kujua, Wananchi wapewe ushauri wa kitaalam katika shughuli zao za uzalishaji ili kupata tija, , Watumishi waache ubinafsi wa kujifikiria wao na maisha yao pekee bali wabadilike kifikra kumfikiria Mwananchi maskini wa hali ya chini kwa sababu lengo la Taifa ni kuinua kipata chake, Kila Mtumishi aoneshe malengo na mpango kazi wake na aoneshe ubunifu wake katika utekelezaji wa mpango kazi wake na kuamini kuwa kila kitu kinawezekana mwisho aliwataka Watumishi wate wanaoishi nje ya Halmashauri ya Mji wa Tunduma wahamie katika eneo la Halmashauri mara moja ili kutoa huduma kwa Wananchi kwa wakati wote watakapohitajika.
Elimu
Mkuu wa mkoa aliagiza kuwa wanafunzi wanaomaliza darasa la Saba wanatakiwa kuendelea hadi kidato cha Nne hivyo Halmashauri ya Mji ihamasishe ujenzi wa Shule za Sekondari zaidi pia alisisitiza umuhimu wa kuongeza ujenzi wa Shule mpya zaidi ili kunufaika na fedha inayotolewa na Serikali.
Pia Chiku Gallawa asisitiza umuhimu wa Wanafunzi kupata chakula shuleni ili kuongeza ufaulu.
Miundombinu
Halmashauri ifuatilie miradi yote kwa ukaribu ili iwe na thamani sahihi ya fedha iliyotumika, Watendaji na Wananchi wasimamie na kutunza hifadhi ya barabara vilevile alisisitiza umuhimu wa ujenzi wa kituo cha Forodha cha Mpakani na kuwataka Wananchi washirikishwe na wanaokataa kuondoa nyumba zao zivunjwe kwa mujibu wa sheria.
Mazingira
Chiku Gallawa aliagiza kuwa Wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu zinazosababisha uharibifu waondolewe mara moja.
Gharama za taka zinatakiwa zitolewe na mzalisha taka mwenyewe na aliwataka Wanachi watunze mazingira yanayowazunguka.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.