Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amehitimisha ziara ya siku tano Mkoani Songwe mapema leo na kusisitiza ushirikiano baina ya uongozi ili kuharakisha maendeleo.
Mhe Samia Suluhu Hassan amesema akiwa ziarani katika wilaya za Momba, Mbozi na Ileje amebaini kuwa Mkoa wa Songwe umebarikiwa kuwa na rasilimali na utajiri mkubwa kinachotakiwa ni viongozi kushirikiana katika kuwatumikia wananchi.
“Nimefurahishwa na kaulimbiu yenu ya maendeleo yataletwa na sisi wenyewe kwa ushindani na ushirikiano, bila ushirikiano hakuna maendeleo, kauli mbiu hii sasa ionekane kwa vitendo”, amesisitiza.
Ameongeza kwa kuwataka watendaji na viongozi wote wapende kuwatembelea wananchi kuanzia ngazi za vijiji ili waweze kuwahudumia vizuri na sio kukaa ofisini.
Mhe Samia Suluhu Hassan ameongeza kwa kuzitaka halmashauri kutenga fedha kwa ajili ya kuwakopesha wanawake na vijana na kubuni miradi mikubwa itayaowaunganisha wajasiriamali wanawake na vijana kutengeneza viwanda ili kuondokana na umasikini.
Amesema mpango wa mkoa wa kuanzisha vituo vya maendeleo vya kata utawezekana na kuwanufaisha wananchi endapo watendaji watajitoa kwa dhati kuufanikisha na mpango huu utaiwezesha Songwe kupaa kiuchumi.
Aidha Mhe Samia Suluhu Hassan amewataka wananchi wa Mkoa wa Songwe kuendelea kutunza mazingira kwa kupanda miti na wale walioko mipakani kuendelea kutunza amani.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa ameshukuru Mhe Samia Suluhu Hassan kwa kufanya ziara mkoani Songwe kuahidi kuwa maelekezo na maagizo aliyoyatoa atayasimamia yatekelezwe.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.