Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kufanya ziara ya siku tano ya kikazi Mkoani Songwe kuanzia Julai 21 mpaka 25, 2018.
Akitoa taarifa kwa umma kupitia vyombo vya habari ofisini kwake, Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa amemshukuru makamu wa Rais kwa kuupa heshima ya kuutembelea mkoa mchanga ukiwa na miaka miwili tangu uanzishwe.
Gallawa amewataka wananchi wa Mkoa wa Songwe kuipokea heshima hiyo kwa kujitokeza kwa wingi kumlaki makamu wa Rais na kuuonyesha ukarimu wao wa kupenda wageni.
“Wananchi wa Songwe tuna jadi yetu ya kupenda wageni, ni matumaini yangu mtajitokeza kwa wingi hususani maeneo yote ambayo Mgeni wetu atatembelea, mtaonyesha utulivu na amani kipindi chote ambacho atakuwa mkoni kwetu kwakuwa hiyo ndiyo desturi ya wana Songwe”, ameongeza Gallawa.
Ameongeza kuwa tarehe 21 Julai, 2018 Mhe Samia Suluhu Hassan atapokea taarifa ya mkoa na kuzungumza na viongozi na watumishi wa mkoa wa Songwe, tarehe 22 Julai, 2018 atakagua na kukifungua kituo cha Afya cha Nanyala pia atakagua na kuweka jiwe la msingi mradi wa maji Katika kijiji cha Iyula Wilayani Mbozi.
Gallawa amesema tarehe 23 Julai, 2018 Mhe Samia Suluhu Hassan atakuwa Wilaya ya Momba katika halmashauri ya Tunduma ambapo atazungumza na watumishi wote, atakagua na kuzindua Kituo cha Afya cha Tunduma na pia atakagua shughuli za wajasiriamali wa Tunduma.
“Akiwa Wilayani Ileje tarehe 24 Julai, 2018, Mhe Samia Suluhu Hassan atazungumza na watumishi wote, atapokea taarifa ya shughuli za uhifadhi wa mazingira na upandaji wa miti pamoja na kukagua shughuli za uhifadhi na shamba la miti la TFS Katengele”, ameongeza Gallawa.
Gallawa ameeleza kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan atahitimisha ziara yake ya siku tano mkoani songwe tarehe 25 Julai, 2018 kwa kufanya kikao cha majumuisho Wilayani Mbozi na viongozi wote wa mkoa wa Songwe.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.