Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Samia Suluhu Hassan amezindua shamba la miti la Iyondo Msimwa lililoko katika kijiji cha Katengele wilayani Ileje lenye hekta zaidi ya elfu 12 na miche zaidi ya laki nne.
Mhe Samia Suluhu Hassan amefanya uzinduzi huo mapema leo ambapo shamba hilo linatarajiwa kutunza vyanzo vya maji 32, kuwaifadhi mbega ambao wako hatarini kutoweka kutokana na kuwindwa hususani na wenyeji pamoja na kutoa ajira kwa wananchi 400.
Amesema shamba hilo linatarajiwa pia kutoa miche elfu 50 kwa wananchi ili wapande hivyo basi wananchi wachangamkie miche hiyo na kupanda kwenye maeneo yao ili kutunza mazingira yaendelee kubaki mazuri na ya kuvutia kama yalivyo.
“Wananchi wa Ileje mmebarikiwa kuwa na mazingira mazuri, wazazi wenu wasingetunza mazingira haya ninyi msingefaidi hali hii nzuri ya hewa nzuri, maji yanatirirka mnalima vizuri, ndugu zangu wa Ileje hasa wa huku Sange na vijiji vya jirani mmepata Baraka kubwa kutoka kwa mungu muitunze”, ameongeza.
Mhe Samia Suluhu Hassan amesema kuwa amesikitishwa na wananchi kujenga katika milima na kukata miti yote katika maeneo ya milimani hali ambayo itasababisha kukosekana mvua, mito kukosa maji hali itakayopelekea kukosekana kwa maji.
“Tusipotunza mazingira yatatuadhibu, vyanzo vya maji vikiharibiwa pia tutapata magonjwa na maji tutakosa na hiyo ndiyo adhabu yenyewe…, lakini pia tunazo sheria na miongozo inayoongoza utunzaji mazingira ambazo zina adhabu zake kwa yeyote anayeharibu mazingira ata adhibiwa”, amesisitiza.
Naye Murugenzi wa Rasilimali misitu kutoka Wakala wa Huduma za Misitu (TFS) Mohamed Kilonzo amesema baadhi ya changamoto za shamba hilo la miti ni pamoja na wananchi kuvamia baadhi ya maeneo ya samba hilo na mifugo kuingia ndani ya shamba hali inaopelekea uharibifu wa miti inayopandwa.
Kilonzo amesema ili kukabiliana na changamoto hiyo TFS imetoa elimu kwa wananchi juu ya madhara ya mifugo kuingia ndani ya hifadhi na wananchi wameanza kuelewa umuhimu wa shamba hilo.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.