Mamia ya wananchi Mkoani Songwe wamejitokeza kupima maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) katika shule ya Sekondari Nalyelye Mlowo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Upimaji VVU na kuanzishiwa dawa za kupunguza makali (ARV) ijulikanayo kama Furaha yangu Pima, Jitambue, Ishi.
Uzinduzi wa Kampeni hiyo ya Furaha yangu umefanywa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemus E Mwangela mwishoni mwa wiki ambapo katika siku hiyo wananchi 367 wamejitokeza kupima VVU, kati yao wanaume 208 na wanawake 159 huku kampeni hiyo ikisisitiza zaidi wanaume kupima VVU kutokana na takwimu kuonyesha wanaume wachache ndio hupima.
“Wanaume tumekuwa na tabia ya kuwatanguliza wake zetu kupima VVU, sasa tufanye tofauti, sisi wanaume ndio tuongoze wafuate akina mama, tukipima tukajua afya zetu tutaweza kuishi kwa furaha, hata ukibainika kuwa na maambuzi ya VVU utaanzishiwa dawa mara moja hii itasaidia kuimarisha afya yako na utaendelea kuishi kwa furaha”, amesisitiza Brig. Jen. Mwangela.
Ameongeza kuwa wananchi wajenge tabia ya kupima afya zao hata katika magonjwa mengine kama ambavyo imefanyika katika uzinduzi wa kampeni hiyo ambapo wananchi 320 walijitokeza kupima kisukari na shinikizo la damu, wanaume 30 walijitokeza kufanyiwa tohara na katika kuchangia damu zilipatikana chupa 34.
Kwa upande wake Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Kheri Kagya amesema kampeni ya Furaha yangu imetoa picha ya kuwa wananchi wengi bado wana uhitaji wa kupima VVU na magonjwa mengine yasiyo ambukiza ili wapate huduma mapema kabla hawajapata madhara makubwa, hivyo basi kila halmashauri zitaweka utaratibu wa upimaji afya angalau mara moja kwa mwezi kwa kuwafuata wananchi katika ngazi za vijiji na kata.
Dkt Kagya amesema hamasa kubwa ilifanyika kwa njia mbalimbali na wananchi walihamasika kufika kwenye uzinduzi kwa wingi na pia kujitokeza kupima kwa wingi, matumaini ya Mkoa ni kuwa wananchi wameelewa kuwa furaha yangu ni kupima VVU kutambua hali zao za kiafya ili waishi kwa amani na furaha
Mkazi wa Mlowo Wilfred Myatege aliyejitokeza kupima amesema kupima afya ni muhimu kwa kila mmoja kwa kuwa mtu anaweza kuwa na magonjwa na asijitambue mapema mpaka madhara makubwa yatakapojitokeza.
Myatege ameongeza kuwa wananchi wengine hudhani kuwa wamerogwa baada ya kupata madhara ya magonjwa ambayo wangeyatambua mapema wasingedhurika sana, hivyo basi fursa hiyo ya upimaji waitumie vizuri kutambua hali zao mapema.
Katika kipindi cha mwaka 2016 watu 71,000 walijitokeza kupima VVU Mkoani Songwe ambapo wanaume walikuwa asilimia 41.4 na katika kipindi cha mwaka 2017 waliopima VVU ni 129,853 wanaume walikuwa asilimia 45.6 ambapo asilimia ya maambukizi ilikuwa 5.8.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.