Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania Inmi Patterson ameahidi kuwa Marekani itaendeleza ushirikiano mzuri na Mkoa wa Songwe pamoja na nchi ya Tanzania, mara baada ya kuwasili mkoani hapa kwa ajili ya ziara ya siku mbili.
Kaimu Balozi Patterson ametoa ahadi ya ushirikiano alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus E. Mwangela ofisini kwake na kuongeza kuwa ana shukuru uongozi wa Mkoa kwa kudumisha ushirikiano mzuri.
“Serikali ya Marekani iko pamoja na serikali ya Tanzania katika kujenga Tanzania yenye elimu bora, afya bora na lishe bora, tunaahidi ushirikiano zaidi na mkoa wa Songwe”, amesema.
Kaimu Balozi Patterson ameongeza kuwa kuna miradi mbalimbali ambayo inafadhiliwa na nchi hiyo hivyo ziara yake pia imelenga kuimarisha ushirikiano katika miradi hiyo ili itekelezwe vizuri.
“Nilisikia mkoa umepata kiongozi mpya nikaona nifanye haraka kuja huku ili kwa pamoja tuendeleze ushirikiano mzuri na miradi mbalimbali tunayotekeleza huku ifanyike vizuri”, amesisitiza Kaimu Balozi Patterson.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus E. Mwangela amesema ziara ya Kaimu Balozi Patterson imekuwa nzuri kwakuwa Kaimu balozi huyo amepata taarifa za miradi wanayofadhili na kuahidi kuendelea kufadhili miradi mingine.
Brig. Jen. Mwangela amesema Kaimu Balozi Patterson ameguswa na tatizo la udumavu katika Mkoa wa Songwe na ameahidi kusaidia katika eneo la lishe, aidha miradi mingine ambayo ameahidi ushirikiano ni ya elimu na kilimo hususani kilimo cha Umwagiliaji.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.