Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Kheri Kagya ametoa rai kwa wananchi wote Mkoani Songwe kuwa na tabia ya kufanya mazoezi ya viungo mara kwa mara ili kuufanya mwili ubaki na uzito unaotakiwa na hivyo kupunguza magonjwa yasiyo ambukiza.
Dkt Kagya amesema hayo wakati wa mazoezi ya Viungo yaliyoongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela katika Wilaya ya Ileje lengo likiwa kuhamasisha wananchi kujenga mazoea ya kufanya mazoezi mara kwa mara.
Amesema kwa sasa kumekuwa na ongezeko kwa asilimia 33 la vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyoambukiza kama vile shinikizo la damu na kisukari ambavyo hupatikana hasa kwa kutofanya mazoezi mara kwa mara.
“Mazoezi ni nyenzo muhimu ya kuzuia magonjwa yasiyoambukiza na inashauriwa angalau kwa siku mtu ufanye mazoezi kwa dakika 30 na waliojitokeza kufanya mazoezi leo wasiache kwani watapata maumivu makali na pia hawataweza kuiona faida ya mazoezi katika afya zao”, amesema Dkt Kagya.
Dkt Kagya ameongeza kuwa miaka ya 1990 vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ambukiza vilikuwa asilimia 19 lakini sasa vifo hivyo vimefikia asilimia 33 na hii imesababishwa na watu kuacha misingi ya kufanya mazoezi ya mara kwa mara.
“Ongezeko la vifo vitokanavyo na magonjwa yasiyo ambukiza linasababishwa na kuacha misingi ya mazoezi, vitambi sio dili tena, tufanye mazoezi ili kupunguza uzito usiohitajika kwani kwa sasa tunao watu wengi wenye uzito ulio zidi wastani na uliopitiliza”, amesisitiza Dkt Kagya
Ameongea kuwa mazoezi ni muhimu ili kujenga afya bora ya mwili na akili na hasa akina mama wengi ambao wamekuwa wakihisi kuwa mazoezi ni kwa ajili ya wanaume tu, hivyo basi wasisubiri matukio bali wafanye mazoezi mara kwa mara kwani afya bora ni mtaji wa kufikia uchumi wa kati.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amewashukuru wananchi wa Mkoa wa Songwe hususani wa Wilaya Ileje waliojitokeza kwa wingi kufanya mazioezi ili kujenga afya zao.
Brig. Jen. Mwangela amesema mazoezi hujenga afya bora na uhusiano mzuri hivyo anawapongeza wote walioshiriki hususani wanawake na watoto walioshiriki kuanzia mwanzo wa mbio (jogging) mpaka mwisho wapewe hamasa ya kuendelea na mazoezi.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ileje Jonas Mkude amemshukuru Mkuu wa Mkoa wa Songwe kwa kuhamasisha wananchi Kufanya mazoezi ili kuboresha afya zao.
Mkude amesema wananchi wa Ileje wanapenda mazoezi na Michezo hivyo wataendelea kufanya mazoezi mara kwa mara ili kujenga afya na kukuza michezo Wilayani humo.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.