Miradi ya maendeleo 27 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 7 inatarajiwa kuzinduliwa, kutembelewa na kuwekewa mawe ya msingi na Mwenge wa uhuru katika mkoa wa Songwe.
Katika sekta za elimu, afya, barabara, maji, kilimo na ufugaji miradi itakayozinduliwa na mwenge wa uhuru itaboresha utoaji na upatikanaji wa huduma, huku uwekaji wa mawe ya msingi na kutembelewa kwa miradi hususani ya ujenzi utawezesha kukamilika miradi hiyo kwa muda uliopangwa na kwa ubora unaotakiwa.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa ameeleza kuwa mchango wa nguvu za wananchi ni shilingi milioni 391 katika miradi hiyo ambayo ni chachu ya maendeleo kwa mkoa wa Songwe huku fedha kutoka serikali kuu ni bilioni 4, fedha za mapato ya ndani kutoka halmashauri milioni 555 na fedha kutoka kwa wahisani bilioni 1.4.
Aidha, Gallawa ameupokea mwenge wa uhuru kutoka mkoa wa Rukwa Mei 11, 2018 na kubainisha kuwa vijiji 38 na halmashauri zote tano zitapitiwa na mwenge wa uhuru kwa umbali wa kilomita 619.9, kisha kukabidhiwa mkoani Mbeya Mei 16, 2018.
Ujumbe wa mbio za mwenge wa uhuru kwa mwaka 2018 ni “Elimu ni Ufunguo wa Maisha; Wekeza sasa kwa maendeleo ya taifa letu”, pia mbio za Mwenge wa Uhuru zinahimiza masuala mengine muhimu ya Kitaifa ambayo ni Mapambano dhidi ya Dawa za Kulevya kwa kauli mbiu ‘Tuwasikilize na Kuwashauri Watoto ili Wasitumie Dawa za Kulevya’.
Jumbe nyingine ni Mapambano dhidi ya Rushwa kwa kauli mbiu ‘Kataa Rushwa, Jenga Tanzania’, Mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI kwa kauli mbiu ‘Mwananchi Jitambue, Pima Afya yako sasa’ na Mapambano dhidi ya Malaria kwa kauli mbiu, ‘Shiriki Kutokomeza Malaria kwa Manufaa ya Jamii’.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.