Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Francis Michael, ametoa maelekezo mahususi kwa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Mkoa huo kuhusu matumizi ya magari ambayo yametolewa na serikali kwa ajili ya usimamizi wa shughuli za afya na kubebea wagonjwa. Maelekezo hayo yalitolewa leo Februari 20, 2024, wakati wa hafla ya makabidhiano ya magari 10 kwa wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa wa Songwe Makabidhiano hayo
yamefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wilayani Mbozi Mbozi.Dkt. Francis amewaagiza Wakurugenzi hao kuhakikisha kuwa magari hayo yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na si kwa shughuli nyingine yoyote. Amesema, "Hatutarajii kuyaona magari ya wagonjwa yakitumika kwa shughuli nyingine tofauti na kusafirisha wagonjwa.
"Aidha, amewataka Wakurugenzi hao kutenga bajeti kwa ajili ya kufanya matengenezo endelevu ya magari hayo ili kuepusha kuchakaa mapema na kushindwa kufanya kazi. Amesisitiza umuhimu wa matumizi sahihi ya magari hayo katika kukabiliana na changamoto za vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga vinavyotokea kutokana na kuchelewa kusafirishwa kutoka vituo vya ngazi ya chini kwenda kwenye vituo vinavyotoa huduma za dharura.
Dkt. Francis ameeleza kuwa, kati ya magari hayo 10, manne ni kwa ajili ya usimamizi katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa, Hospitali ya Rufaa ya Mkoa, pamoja na timu za usimamizi za Wilaya za Songwe na Ileje. Magari sita yatapelekwa katika kila jimbo kwenye Halmashauri zote za Mkoa wa Songwe. Mkoa huo bado unatarajia kupokea magari matatu mengine kwa ajili ya timu za usimamizi katika Halmashauri za Wilaya za Mbozi na Momba, pamoja na Halmashauri ya Mji Tunduma.Kabla ya kupokea magari hayo 10, Mkoa wa Songwe ulikuwa na magari 13 tu, ukilinganisha na mahitaji halisi ya magari 30 kwa ajili ya shughuli za usimamizi wa huduma za afya na kubebea wagonjwa, alisema Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Boniphace Kasululu.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.