Mpango wa uongezaji virutubishi katika unga wa mahindi umezinduliwa rasmi Mkoani Songwe huku Mkuu wa Songwe Chiku Gallawa akiwataka wataalamu na taasisi zinazohusika na lishe kusimamia suala la ubora wa chakula kwakuwa linagusa maisha ya binadamu.
Gallawa amesema mpango huo utasaidia kupunguza kiwango cha udumavu ambacho kwa sasa ni asilimia 37.7 hali ambayo haikubaliki kutokana na uwepo wa vyakula vya kutosha mkoani hapa.
“Mkoa wa Songwe kubaki na asilimia kubwa ya udumavu, utapiamlo na ukondefu haikubaliki, vyakula vipo, kilichobaki ni wataalamu wa lishe kufanya kazi yenu ya kuelimisha namna ya kuchanganya vyakula hivyo vilete afya bora na mafunzo hayo yafike mpaka ngazi ya vijiji”, amesisitiza Gallawa.
Ameongeza kuwa masuala ya chakula yanagusa usalama wa wananchi hivyo Mkoa wa Songwe umejipanga kufikia malengo ya maendeleo hasa kwa kutumia taarifa, takwimu sahihi na mipango inayotekelezeka.
“Hatutaki maneno ya ubabaishaji, tunahitaji takwimu na taarifa sahihi, tumejipanga kuelekea kwenye uchumi wa viwanda utakaojengwa na wananchi wenyewe wakiwa na afya bora hivyo basi taasisi zote zinazohusika na masuala ya chakula mkija Songwe muwe na mikakati inayotekelezeka”, amefafanua.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mradi wa NAFAKA nchini Silas Ng’habi amesema malengo ya mradi wa uongezaji virutubishi unoafadhiliwa na shirika la kimataifa la USAID ni kuwapa wananchi chakula kilicho bora.
Amesema viinilishe vitakavyowekwa katika unga wa mahindi vitajenga jamii yenye afya bora na hivyo kupata wabunifu wa teknolojia mbalimbali pamoja na kuwajenga watoto wenye ufahamu mkubwa.
Naye Afisa Lishe kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Elizabeth Ndaba amesema kuwa virutubishi vitakavyoongezwa katika unga wa mahindi ni salama kwakuwa vimekaguliwa na kuhakikiwa na shirika la viwango nchini (TBS) ili kuangalia ubora wake pamoja na Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA) Kuangalia usalama kwa watumiaji.
Ndaba amesema mpango wa uongezaji virutubishi umelenga kupunguza hali ya udumavu nchini ambayo ni asilimia 34 huku akifafanua kuwa udumavu hudhoofisha afya ya mwili na uwezo wa kiakili hali ambayo pia huathiri katika uzalishaji na ukuaji wa uchumi nchini.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.