Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa amewahakikishia wanawake wa kijiji cha Saza Wilaya ya Songwe kuwa wanaweza kufanya kazi ya kuchimba madini hivyo wachangamkie fursa hiyo.
Gallawa ameyasema hayo mapema leo alipowatembelea wanawake waliokuwa wakipewa elimu ya uchimbaji madini katika kijiji cha Saza ambapo baadhi yao walionekana kuwa na mashaka endapo mwanamke anaweza kuingia ndani ya mgodi na kuchimba madini.
“Nimeshuhudia kwa macho yangu wanawake wanachimba madini tena kwa kutumia sululu, ninyi mtashindwa kweli?!, wanawake wana nguvu na akili nyingi, msijishushe hakuna kazi ya mwanaume na mwanaume, sasa hivi kuna wahandisi wanawake kila idara, marubani na viongozi wakubwa tu”, amesisitiza Gallawa.
Ameongeza kuwa mara baada ya mafunzo hayo ya Afya na Mazingira, usalama migodini na sheria za madini wanawake hao wanapaswa kujiunga katika vikundi ili serikali iweze kuwafikia kwa urahisi.
“Najua wanawake wengi tuna historia ya kufanya vizuri kwenye vikundi naimani baada ya mafunzo haya mtajiunga kwenye vikundi na ninamuagiza afisa maendeleo ya jamii arudi tena kutoa mafunzo ya ushirika ili muelewe vizuri”, amefafanua Gallawa.
Gallawa amesema vikundi hivyo vitasaidiwa kuandaa andiko la mradi, kuwapa mafunzo Zaidi, kupatiwa leseni na mitaji yao ambayo itakuwa mikopo kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Madini na mifuko mbalimbali.
Naye Mkazi wa Kijiji cha Saza Wilaya ya Songwe Bi Elimina Atanasi ameiomba serikali licha ya kutoa mafunzo hayo ya uchimbaji, itenge maeneo ya uchimbaji kwa ajili ya wachimbaji wadogo hasa vikundi vya akina mama.
Bi Atanasi amesema wachimbaji hao wadogo hasa wanawake wamekuwa wakipata shida ya kuondolewa katika maeneo wanayochimba jambo ambalo linawafanya wakose fedha za kukidhi mahitaji yao.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.