RAS SENEDA ATAKA MIGOGORO YA ARDHI ITATULIWE NA HALMASHAURI KABLA HAIJAFIKA MKOANI.
SONGWE: Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda amewagiza viongozi wa Halmashauri kwa kushirikiana na watalamu wa Ardhi kutatua migogoro yote ambayo ipo kwenye maeneo yao kabla haijafika ngazi ya Mkoa.
Katibu Tawala wa Mkoa ametoa maagizo hayo wakati wa kikao kazi cha sekta ya Ardhi kilichowakutanisha watalamu wote wa Ardhi pamoja na wakurugenzi wa Halmashauri zote za Mkoa kilichofanyika Septemba 23 Mkoani Nselewa.
Bi. Happiness Seneda amesema migogoro yote ya Ardhi inatakiwa kutatuliwa na Halmashauri kwani Mkoa hauna Ardhi isipokuwa tu kwa migogoro ambayo Mkoa unaweza kushauri au kufanya jambo ili kumaliza mgogoro wa huo.
Katika kufanikisha utatuzi wa migogoro ya Ardhi lazima tufanye kazi kama timu moja kwa ushirikiano mkubwa hakuna mtu wa kujiona yeye ndio yeye.
Serikali itafuatilia kwa karibu sana kuona kama mnafanya kazi kama timu na kwa kushirikiana, kwani eneo la Ardhi ndio kipaumbele chetu amesema, Bi. Happiness Seneda.
Pia, Bi. Happiness Seneda amesema anataka kuona eneo la Mkoa linapimwa na kupangika vizuri kwa kutumia fedha za Serikali au kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Watalamu wa Ardhi kutoa ushirikiano mzuri kwa mtu mwenye eneo lake ambaye anahitaji lipimwe ili tuweze kuongeza maeneo mengi yaliyopimwa na tusiwatie hofu juu ya gharama kubwa za upimaji ila tuwape mbinu bora na nzuri za kufanikisha, amesema, Bi. Happiness Seneda.
Aidha, Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda ameziagiza Halmashauri zilizopata fedha za upimaji viwanja kuanza kurejesha fedha izo ili zikafanye kazi nyingine za Serikali.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Tunduma, Ndg. Philemon Magesa ametoa wito kwa watalamu wa Ardhi kushirikiana kwa Karibu na ofisi za wakurugenzi ili waweze kutatua changamoto kwa pamoja, na wasiwe watu wa kujitenga kujiona wao sio sehemu ya Halmashauri.
Ndg. Magesa amesema swala la kupima Ardhi, watalamu wa Ardhi wakiamua na kujituma kwa ushirikiano na Mkurugenzi wanaweza kupima Ardhi eneo kubwa sana kwa kutumia Rasilimali zilizopo.
"Mfano Tunduma tumeweza kutumia fedha za mapato ya ndani zaidi ya milioni 15 na tumefanikiwa kupima viwanja zaidi ya 600 hivyo jambo ili linawezekana swala watalamu wa Ardhi wasiwe mbali na Halmashauri" Philemon Magesa.
Aidha, Ndg. Magesa amesema watalamu wa Ardhi wakijipanga vizuri wanaweza kutatua migogoro yote na ikaisha, kama sisi Tunduma tulianza kuunda timu ya kuitambua na migogoro yote ya Ardhi na kuisajili, tumeitambua na tumeanza kuchukua hatua za kutatua kwa wananchi kuwapatia viwanja kwenye mpango huu ambao tumeanza kupima.
Kaimu Kamishina wa Ardhi Mkoa wa Songwe, Winfrida Mwasulama amewataka watalamu wenzake kufanya kazi kwa ushirikiano ili kufanikisha kwani kazi za Ardhi mtu moja asipotekeleza jukumu lake vizuri basi mwingine naye hawezi kufanya kwa ufasaha.
Kwa upande wake, Kamishina wa Ardhi Mkoa wa Mbeya, Syabumi Mwaipopo amewataka wakuu wa Idara za Ardhi kuwatumia vizuri vijana wanaojitolea ili kuweza kutekeleza majukumu vyema ya Mipango ya Ardhi.
Wakati huo huo, Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda amesisitiza ukusanyaji wa Kodi ya Ardhi na kuwataka watalamu wa Ardhi kuwakunbusha wananchi juu ya msamaha uliotolewa na Serikali kwa wanaodaiwa Kodi ya Ardhi.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.