Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas Elias Mwangela amewasili katika ofisi yake mapema leo asubuhi kufuatia kuteuliwa kwake kuuongoza Mkoa wa Songwe na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe John Pombe Magufuli Julai 28, 2018.
Brigedia Jenerali Mwangela amepokelewa na kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya nne za Mkoa wa Songwe, wakurugenzi wa halmashauri tano za Mkoa huu, wakuu wa idara pamoja na watumishi wote wa ofisi yake.
Mara baada ya mapokezi hayo Brigedia Jenerali Mwangela amepokea taarifa ya makabidhiano kutoka kwa aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Luteni Mstaafu Chiku Gallawa katika kikao cha pamoja na wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wakuu wa idara na wajumbe wa kamati ya ulinzi na Usalama.
Gallawa amesema kuwa anayo furaha kumkaribisha Brigedia Jenerali Mwangela na anamshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe John Pombe Magufuli kwa kumteua Brigedia Jenerali Mwangela, na kuwa wale waliokuwa wakifurahia kuondoka kwake wakijua sasa wataanza kufanya kazi ndivyo sivyo wajue wamepata kiongozi ambaye ni makini zaidi”.
Ameongeza kwa kuwataka watendaji na wanasiasa waendelee kuchapa kazi kwa bidii wakiwa na lengo la kumkomboa mwananchi wa Songwe kutoka katika umasikini na kuongeza pato la mkoa na taifa.
Naye Brigedia Jenerali Mwangela amemshukuru Gallawa kwa kuweka misingi mizuri ambayo imelenga kuuinua Mkoa wa Songwe kiuchumi na kuahidi kuwa atahakikisha mazuri yote atayaendeleza hasa pale alipoishia.
Ameongeza kwa kuwasihi watendaji kufanya kazi kwa kufuata sheria, taratibu na maadili ya utumishi wa umma na kwa kushirikiana kwa kuwa anaamini katika ushirikiano kazi zinafanyika kwa ufanisi.
"Tufanye kazi tuwatumikie wananchi wa Songwe, milango ya ofisi yangu itakuwa wazi kwenu kwakuwa napenda kufanya kazi kwa ushirikiano, nami pia ninaomba ushirikiano wenu kama mliokuwa mnapa Gallawa ikiwezekana hata Zaidi,” amesema Brigedia Jenerali Mwongela.
Amewataka watumishi kuzingatia muda katika kila jambo wanalotekeleza wasiopoteze muda huku akiwasisitiza kufanya kazi kama timu moja.
“Nawapa mfano wa silaha ya mzinga ambao ili iweze kufanya kazi vizuri wanahitajika watu sita ambao kila mmoja ana jukumu lake la kufanya ili mzinga huo ufanye kazi kwa ufanisi, hii ni timu na akikosekana mmoja mzinga hautaweza kufanya kazi sawasawa, nasisi tuige ushirikiano kama huu kila mmoja atekeleze jukumu lake ili tufikie lengo moja”, amefafanua Brigedia Jenerali Mwangela
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.