Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mheshimiwa Jabir Omari Makame, leo amefungua rasmi Jukwaa la Wadau wa Kilimo la Mkoa wa Songwe, hafla iliyowakutanisha wataalam, viongozi wa taasisi mbalimbali, wakulima, wawekezaji na wadau wengine muhimu wa sekta ya kilimo. Tukio hilo limefanyika kwa lengo la kujadili kwa pamoja nafasi, changamoto na fursa zilizopo katika sekta hiyo ili kuongeza tija na kuinua uchumi wa wananchi wa Songwe.
Katika ufunguzi huo, Mheshimiwa Makame amesisitiza kuwa sekta ya kilimo ndiyo mhimili mkuu wa uchumi wa mkoa, hivyo jukwaa hilo linafungua ukurasa mpya wa mipango shirikishi itakayowezesha mkoa kuongeza uzalishaji, uongezaji wa thamani na masoko ya uhakika.
Katika jukwaa hilo, washiriki wanatarajiwa kujadili kwa kina hali ya sekta ya kilimo katika Mkoa wa Songwe, ikijumuisha fursa zilizopo, changamoto zinazowakabili wakulima pamoja na hatua zinazohitajika ili kuongeza tija katika uzalishaji. Aidha, tathmini ya uzalishaji wa mwaka 2025 pamoja na mpango wa uzalishaji wa mwaka 2026 itawasilishwa, sambamba na maandalizi ya msimu ujao wa kilimo kwa mwaka 2026 ili kuhakikisha mkoa unaendelea kuwa kinara katika uzalishaji wa mazao ya kimkakati.
Vilevile, jukwaa litajadili masuala yahusuyo usindikaji wa mazao, uongezaji wa thamani, biashara, masoko pamoja na upatikanaji wa mitaji, ambapo wadau mbalimbali wataeleza namna mnyororo wa thamani wa mazao unavyoweza kuimarishwa ili kumpa mkulima kipato zaidi. Kadhalika, mada kuhusu kilimo hifadhi na mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi itazungumziwa, ikilenga kuwajengea wakulima uelewa wa matumizi ya mbinu rafiki kwa mazingira na kuhimili athari za mabadiliko ya hali ya hewa.
Mkuu wa Mkoa amehimiza wadau wote kutumia jukwaa hilo kama chombo cha kuweka mikakati thabiti ya kubadilisha sekta ya kilimo kuwa ya kisasa na yenye ushindani, ili kuongeza kipato cha wananchi na kuchangia ukuaji wa uchumi wa mkoa wa Songwe.




2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.