Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela leo ameingia mkataba na wakuu wa Wilaya zote nne za Mkoa wa Songwe kwa ajili ya utendaji kazi na usimamizi wa Huduma za Maji na Usafi wa Mazingira.
Mara baada ya kusaini mikataba hiyo Brig. Jen, Mwangela amewaeleza kuwa mkataba huo uanze kuonyesha mabadiliko ndani ya miezi sita ili baada ya miaka minne ya mkataba kumalizika kila wilaya iwe na mazingira safi ikiwa ni pamoja na kila mwananchi kuwa na choo bora.
Amesema katika kutekeleza mkataba huo shirika la UNICEF wameahidi kushirikiana na Mkoa wa Songwe ili kufikia malengo kwani wameona nia na mipango madhubuti ya kuhakikisha usafi wa mazingira unakuwa kipaumbele kwa mkoa wa Songwe.
“Katika kutekeleza mkataba huu nitakuwa nawapima wakuu wa Wilaya kwa kutumia vigezo vilivyoandaliwa na wataalamu ili tujue nani anafanya vizuri, nitapita katika vijiji tena kwa kushtukiza, nitakagua nyumba za viongozi wa vijiji, sokoni, shuleni na nitaongea na kamati zilizoundwa nitapima na nitatoka na majibu”, amesema Brig. Jen. Mwangela.
Brig. Jen. Mwangela ameongeza kuwa suala la usafi linazuia magonjwa mengi ambayo yanaweza kuepukika huku akielekeza ifikapo mwisho wa mwaka huu kila halmashauri ihakikishe kuna vijiji ishirini vya mfano vyenye vyoo bora na vinazingatia usafi wa mazingira.
Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Dkt Seif Shekalage amesema mkataba huo umewekwa ikiwa ni siku chache baada ya timu ya Mkoa kufanya ziara Mkoani Njombe na kujifunza utekelezaji wa Kampeni ya Usafi wa Mazingira hivyo viongozi wote wana elimu ya kutosha.
Dkt Shekalage amesema mara baada ya Mkataba huo kusainiwa wakurugenzi wafikishe ujumbe wa usafi wa mazingira kwa watendaji wa Halmashauri ili kila mmoja atimize wajibu wake.
Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa Wilaya za Mbozi, Songwe na Ileje Mkuu wa Wilaya ya Momba Juma Irando amesema wao wako tayari kushirikiana na kila anayehusika ili kufanikisha kampeni ya usafi wa mazingira na wako tayari kwa kazi.
Irando ameongeza kuwa wanamuunga mkono Mkuu wa Mkoa na wako tayari kujitoa ili kufanikisha hilo huku akiwashukuru UNICEF kwa ushirikiano ili kuhakikisha Mkoa wote wa Songwe unafanikiwa katika masuala ya usafi wa mazingira.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.