SENEDA: AZITAKA HALMASHAURI KUWEKA RATIBA YA KUSIKILIZA KERO ZA WANANCHI
SONGWE: Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda amezitaka Halmashauri zote za Mkoa wa Songwe kuweka ratiba ya wazi kwa wananchi ya kusikiliza kero zao.
Katibu Tawala Mkoa ametoa maagizo hayo Agosti 10, alipokutana na watumishi wa Halmashauri ya Mji Tunduma na Halmashauri ya Mbozi kwa lengo la kufahamiana baada ya kuhamia Mkoa wa Songwe akitokea Mkoa wa Iringa.
Bi. Happiness Seneda amesema anataka kuona ratiba ya wazi inayofahamika kwa wananchi na iwekwe kwenye mbao za matangazo, tovuti na sehemu yeyote ambayo wananchi wanaweza kuiona ili wajue ni siku gani Halmashauri yao inasikiliza kero zao.
"Nataka kuona timu ya kusikiliza kero ipo au mtu maalumu wa kusikiliza kero na nijue ni lini kero za wananchi zinasikilizwa na ziwe kwenye kumbukumbu na nione wananchi wanapata mrejesho wa kero walizowasiliaha" Bi. Happiness Seneda
Katibu Tawala Mkoa, amesema hataki kuona mwananchi amewasilisha kero yake na inachukuliwa kawaida tu, anahitaji kuona kero yake inasikilizwa hadi mwisho na apate mrejesho wa kero yake.
Halmashauri zote zikitimiza wajibu wao wa kusikiliza kero za wananchi basi kero hizo haziwezi kufika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa kwani Mkoa haumiliki ardhi au wananchi bali wote wako chini ya Halmashauri husika, amesema Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda.
Pamoja na kusikiliza kero za wananchi Pia, Katibu Tawala Mkoa Songwe, Bi. Happiness Seneda amezielekeza Halmashauri kusikiliza kero na changamoto za watumishi ili kujua watumishi wake wanakumbana na changamoto zipi.
Haipendezi mtumishi yuko hapa ana kero na changamoto nyingi lakini sisi kwa sisi watumishi tunashindwa kuzitatua, hii haikubaliki.
Wakati huo huo ameziagiza Idara ya elimu na afya ambazo ndio zina watumishi wengi kuwatembelea watumishi wao na kutatua kero zinazowakabili na kuwatia moyo juu ya ufanyaji kazi.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.