SONGWE IKO SALAMA, TUENDELEE KUCHUKUA TAHADHARI YA EBOLA.
Na. Nicholas Ndabila.
SONGWE: Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Waziri Kindamba amesema mkoa uko salama dhidi ya ugonjwa wa Ebola lakini Serikali bado inaendeleea kutoa elimu dhidi ya Ugonjwa huo hatari wakati nao wananchi wakiendelea kuchukua hatua.
Mhe. Waziri Kindamba ameyasema hayo kwenye kikao kazi cha tahimini utoaji wa chanjo mbalimbali kwa binadamu, kilichofanyika 5 Oktoba 2022 Mkoani na kuhudhuriwa na viongozi ngazi ya Wilaya, Halmashauri pamoja na watalamu wao wa masuala ya Afya.
"Mpaka sasa hakuna Mtu aliyegundulika kuwa na ugonjwa wa Ebola au dalili zake bado iko haja kubwa ya kuendelea kuchukua tahadhari na kujikinga dhidi ya ugonjwa huo kwa kuzingatia maelekezo na miongozo kutoka kwa wataalamu" amesema, Waziri Kindamba.
Mkuu wa Mkoa amesisitiza kuwa kutokuwa na Mgonjwa au mtu mwenye dalili za ugonjwa haina maana tuendelee kubweteka tunahitajika kuendelea kuchukua hatua zaidi za kujikinga kwa kuwa Songwe ni moja ya Mikoa inayo pakana na nchi jirani amabazo wasafiri wanaweza kusafiri mpaka mkoani kwetu na kuhatarisha Taifa letu.
Pia, Mkuu wa Mkoa, Mhe. Waziri Kindamba amewaagiza wakuu wa Wilaya kufuatilia kwa ukaribu zaidi wakishirikiana na wataalamu wao wa Afya, kuhakikisha Mkoa unaendelea kuwa salama kwa magonjwa yote ya mulipuko pamoja na ulinzi na usalama.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Boniface Kasululu amezitaja baadhi ya dalili za ugonjwa wa Ebola ikiwa ni pamoja na kupanda kwa joto la mwili kupita kawaida na kutokwa na damu sehemu za wazi.
"Ni muda kwa wananchi kujiepushe na baadhi ya vitendo vinavyosababisha kuenea kwa ugonjwa wa Ebola kama kula nyama za wanyama poli aina ya Popo,Tumbili na Sokwe, kujiepushe na mikusanyiko isiyo kuwa na ulazima, kuepuka kugusa Mate, Jasho, Kamasi na Kinyesi, kutumia Nguo, Godoro na vifaa vya mtu mwenye maambukizi au mtu mwenye dalili za ugonjwa wa huo" Dkt. Boniface Kasululu.
Hata hivyo amewataka wananchi kuchukua tahadhali wakati wa kuosha maiti ya mtu aliye fariki kwa dalili tajwa hapo juu.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.