SONGWE KUUNDA KIKOSI KAZI KUONGEZA WANACHAMA WA CHF
Uongozi wa Mkoa wa Songwe umejipanga kuunda kikosi kazi cha kuhamasisha makundi mbalimbali ya jamii kama vile Bodaboda, Mama ntilie, waliopo kwenye vyama kama SACOS pamoja na makundi mengine kujiunga na Bima ya Afya ya Jamii iliyoboreshwa (CHF) hili kuweza kuongeza wanachama zaidi 25% kutoka 1.6% iliyopo sasa ifikapo Disemba 2020.
Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Dr. Self Shekalaghe wakati wa kikao kazi na watumishi wanaohusika na uandikishaji wa CHF iliyoboreshwa, wadau wa Afya, Makatibu wa Afya pamoja na Waganga wakuu wa Halmashauri kilichofanyika ukumbi wa Vwawa Sekondari, 17 Novemba 2020.
Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Dr. Self Shekalaghe amesema kwa sasa Mkoa kitaifa uko nafasi ya 24 katika uandikishaji wa CHF na tumefika 1.6% tu sawa na Kaya 3,300 ambazo zimeandikishwa wakati lengo la Kitaifa ni kila Mkoa ufike 30% ya kuandikisha wanachama wa CHF.
“Pamoja na kuunda kikosi kazi cha kuhamasisha makundi mbalimbali tunatafuta wadau mbalimbali waweze kutusaidia kufikia lengo kama ambavyo shirika la HIMSO limetusaidia usafiri wa Pikipiki ambazo watapewa waratibu kila Wilaya hili kuhakikisha uandikishaji wa wanachama wa CHF unaongezeka” Katibu Tawala Mkoa, Dr. Shekalaghe.
Katika kuongeza asilimia za wanachama wa CHF Shirika la HIMSO limechangia pikipiki 4 zenye thamani ya shilingi Milioni 27.1 kwa ajili ya Halmashauri ya Songwe, Ileje, Momba na Tunduma.
Wakati huo huo Katibu Tawala wa Mkoa, Dr. Shekalaghe amesema pikipiki zilizotolewa na Shirika la HIMSO atazigawa kwa Halmashauri husika baada ya kutimiza malengo ambayo watawekeana ya uandikishaji wa wanachama wa CHF kwa muda wa wiki 2 ndio watapewa kwa waliotimiza malengo tu.
Kujiunga na CHF kwa kaya ni Shilingi 30,000 ambayo utaweza kutibiwa katika Zahanati, Vituo vya Afya, Hospitali za Wilaya pamoja na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ndani ya Mkoa wa Songwe tu.
Ikumbukwe Katika CHF ya zamani kufikia Desemba 2018 Mkoa wa Songwe umekuwa kinara kitaifa kwa 76.4% na kufanikisha kaya 198,376 kujiunga na CHF ya zamani
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.