SONGWE YAKAMILISHA MAANDALIZI YA SENSA KWA 96%
SONGWE: Zikiwa zimebaki siku 4 zoezi la Sensa ya watu na makazi kufanyika, Mkoa wa Songwe umekamilisha maandalizi yote na kazi imebaki kwa wananchi kuhesabiwa tu.
Hayo yamebainishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Cosmas Nshenye wakati akimuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Songwe kweye kikao cha Kamati ya Sensa Mkoa kilichofanyika leo Agosti 19.
Mhe. Cosmas Nshenye ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Songwe kujitokeza kwa wingi na kutoa ushirikiano kwa makalani wa Sensa ambao watapita kwenye Makazi yao kwa ajili ya kupata taarifa sahihi za Sensa.
Pia, Mhe. Cosmas Nshenye ametoa wito kwa viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya kitongoji hadi Mkoa kutoa ushirikiano wa hali na Mali kwa makarani watakapokuja wanapita kwenye Makazi yao ili kufanikisha zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Mratibu wa Sensa Mkoa, Ndg. Doto Ibrahim amesema makalani wako tayari kwa kazi ya Kuhesabu watu na makazi kuanzia tarehe 23 Agosti 2022.
Tunajua kabisa Mkoa wetu unapakana na nchi ya Malawi na Zambia ambao wanaingia kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi, hivyo nasi tumejipanga katika maeneo yote ambayo wageni wanafikia ikiwa ni pamoja na sehemu za maegesho ya magari ya Malori ili kuhakikisha wote wanahesabiwa, amesema Doto Ibrahim mratibu wa Sensa Mkoa.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda amesema Serikali imejipanga vizuri kuhakikisha kila mtu anahesabiwa ata kama sehemu iyo kuna migogoro ya mipaka hayawezi kuathiri zoezi la Sensa kwani Sensa ya 2022 inafanywa Kidigitali zaidi.
Pia, ametoa wito kwa wanawake kutoa ushirikiano mzuri kwa makalani kwenye kipengele cha maswali ya uzazi, kwani eneo ilo anapaswa kujibu mwanamke na sio mwanaume, hivyo tunahitaji ushirikiano.
Sheikh wa Mkoa wa Songwe, Sheikh Hussein Batuza ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Mkoa ametoa wito kwa waumini wa dini ya kiislamu na wananchi wote wa Songwe kumuunga mkono kwa vitendo Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluh Hassan kufanikisha zoezi la Sensa ya watu na makazi.
Sensa ya 2022 itakuwa ya kwanza kwa Mkoa wa Songwe tangu uanzishwe 2016 na ni ya sita kwa nchi nzima.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.