Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amesema muda si mrefu Songwe itakuwa kinara katika kutekeleza kampeni ya usafi wa mazingira kwani sasa utekelezaji wa kampeni hiyo unaenda kufanyika kwa kasi na ufanisi mkubwa.
Brig. Jen. Mwangela ameyasema hayo mara baada ya kutembelea vijiji vya Halmshauri ya Wilaya ya Njombe ikiwa ni sehemu ya ziara ya kuona namna walivyotekeleza Kampeni ya Usafi wa Mazingira kwa ufanisi na kuongeza kuwa sasa amebaini siri ya mafanikio yao.
“Nimeona na nimejua siri yao na sasa tumejifunza mengi tunaenda kutekeleza kampeni hii kwa kasi kubwa, tutawashirikisha tuwape elimu wananchi, viongozi wa dini na wa serikali ngazi zote, kila mmoja aweze kuhusika kikamilifu ili wote tuibebe kwa pamoja kampeni hii.”, amesema Brig. Jen. Mwangela.
Ameongeza kuwa katika kutekeleza kampeniya usafi wa mazingira kwa ufanisi watahakikisha wale wasio na uwezo na hawana ndugu wanawekewa utaratibu wa kusaidiwa na uongozi wa vijiji na mitaa ili kila kaya iwe na choo bora na kuweka sheria ili kuwabana wachache watakao kaidi.
Brig. Jen. Mwangela ameongeza kuwa si kwamba Mkoa wa Songwe unafanya vibaya sana katika usafi wa mazingira bali utekelezaji wa kampeni hii unapaswa kufanyika kwa kasi zaidi na ufanisi mkubwa pia ameomba ushirikiano wa wananchi wote waichukue kampeni kwa uzito mkubwa.
Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Dkt Seif Shekalaghe amesema kampeni ya usafi wa mazingira ni ajenda ya kitaifa ambayo ina mipango mikakati inayotumika maeneo yote hivyo wamefanya ziara kujionea namna Mkoa wa Njombe ambao unafanya vizuri kitaifa umetekelezaje mipango hiyo.
Dkt Shekalaghe amesema wamejifunza kuwa Njombe wamefanikiwa kwakuwa walitekeleza kampeni ya usafi wa mazingira kwa ushirikiano mkubwa kuanzia ngazi ya chini, elimu ilitolewa kwa watu wote wakaielewa na kuitekeleza vizuri, kujitoa kwa viongozi pamoja na wananchi kujiwekea sheria ndogo ndogo zinazo elekeza faini kwa wanao kaidi.
Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Matiganjola Wilayani Njombe Erasto Joseph Kapinga amemuambia Mkuu wa Mkoa wa Songwe kuwa wana kijiji wote walipewa elimu ya usafi wa mazingira na mafanikio ya kampeni hiyo ni pamoja na kutokuwepo kwa magonjwa ya tumbo na kuharisha kijijini hapo.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.