Naibu Waziri Kilimo Dkt Mary Mwanjelwa ameupongeza uongozi wa Mkoa wa Songwe kwa kusimamia vema agizo la Waziri Mkuu la kutaka Kahawa kutonunuliwa kwa wakulima bali uuzaji ufanyike katika minada kwa kupitia vyama vya ushirika.
Dkt Mwanjelwa ametoa pongezi hizo mapema jana alipofanya ziara Mkoani hapa na kuzungumza na uongozi wa Mkoa, wakulima na wanunuzi wa kahawa ambapo ameeleza kuwa jitihada za Mkoa wa Songwe zimeonyesha kuunga mkono serikali ya awamu ya tano kwa vitendo.
“Taarifa yenu inaonyesha ongezeko la vyama vya ushirika 17 tangu Waziri Mkuu atoe malekezo hayo mwezi Januari, jitihada hizi zinaonyesha mnaunga mkono jitihada za serikali ya awamu ya tano ya kumkomboa mkulima na mwananchi wa hali ya chini kwa vitendo”, ameeleza Dkt Mwanjelwa.
Ameongeza kuwa elimu juu ya ushirika itolewe kwa wakulima ili wote wajiunge na kuacha kuuza kahawa yao kwa madalali ambao wamekuwa wakiwapunja na hivyo kudhoofisha kilimo cha kahawa.
Dkt Mwanjelwa ameeleza kuwa Wizara yake itaendelea kusimamia na kuhakikisha kuwa mbolea inawafikia wakulima kwa wakati huku akiwataka watendaji kuzingatia maelekezo ya serikali katika usambazaji wa mbolea.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa ameeleza kuwa mkoa unahakikisha Mkulima wa kahawa anafaidika na kilimo hicho kwa kumuelimisha ajiunge na ushirika ili kuepuka madalali ambao wamekuwa wakiwadhulumu.
Gallawa ameeleza kuwa wakulima waliokuwa wamejiunga katika vikundi wataelekezwa namna ya kujiunga katika ushirika ili kutoruhusu watu wachache kufaidi jasho la Mkulima ambaye ndiye mlengwa wa kilimo cha kahawa.
Nao wakulima wa kahawa wa Kijiji cha Isansa Wilaya ya Mbozi wamemueleza Naibu Waziri Dkt Mwanjelwa kuwa wanaunga mkono kauli ya Serikali ya kujiunga katika ushirika kwakuwa wamekuwa wakidhulumiwa na madalali wa zao hilo la kahawa.
Aidha wameitaka serikali kutorudi nyuma katika uamuzi huo wa kuwataka wajiunge katika ushirika huku wakiomba ushirika uboreshwe zaidi ili kuondoa changamoto zilizokuwepo hapo zamani.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.