Disemba 14, 2018
WANAFUNZI WALIOCHAGULIWA KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA 2019
Mkoa wa Songwe umefanya uteuzi wa jumla ya Wanafunzi 16,223 waliofaulu masomo ya elimu ya msingi ili waweze kujiunga na masomo ya sekondari kwa kidato cha kwanza mwaka 2019 ambapo kati ya hao wavulana ni 7,391 na wasichana ni 8,832.
Wanafunzi hao watapangiwa katika shule za sekondari 87 za Mkoa wa Songwe, aidha Mkoa umepewa nafasi za wanafunzi 64 watakaopangiwa shule za bweni za ufundi na kawaida kutokana na ufaulu mkubwa walioupata huku wanne kati yao wenye mahitaji maalumu wamepangiwa shule na Ofisi ya Rais TAMISEMI.
Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Lauteri Kanoni amezitaka Halmashauri zote zikamilishe miundombinu ya vyumba vya madarasa 161 na madawati 8770 ifikapo Disemba 30, 2018 ili kumaliza upungufu uliopo na hivyo wanafunzi wote waliopangiwa waanze masomo shule zitakapofunguliwa.
Kanoni ametoa wito kwa wazazi na walezi kuanza maandalizi mapema na kutumia fedha kwa uangalifu katika msimu huu wa sikukuu ili ifikapo Januari 2019 wawe na akiba kwa ajili ya maandalizi ya wanafunzi hao, pia kuhakikisha wanafunzi wanafika shuleni bila kusubiri msako wa wanafunzi watakaoshindwa kuanza shule.
Naye Afisa Elimu Mkoa wa Songwe Juma Mhina amesema ufaulu kwa Mkoa wa Songwe umepanda kwa asilima 9 huku akieleza kuwa Mkoa umeweka mikakati madhubuti ya kuimarisha elimu msingi ikiwa ni pamoja na kutoa motisha kwa walimu waliofanya vizuri, kuimarisha ufuatiliaji wa ufundishaji wa waalimu na kuhimiza wazazi kuchangia chakula.
Imetolewa na:
Grace Gwamagobe
Afisa Habari Mkoa wa Songwe
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.