Shirika la Umeme Nchini TANESCO Mkoa wa Songwe limepewa siku tatu kuandaa mkakati utakaoeleza namna ya kumaliza matatizo ya umeme ikiwemo katizo la mara kwa mara la umeme na tatizo la kiwango kidogo cha umeme.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. (Mst) Nicodemus E Mwangela ametoa agizo hilo mapema leo asubuhi alipofika ofisi za TANESCO Songwe kufuatia kukatika mara kwa mara kwa umeme na pia kila siku ya Jumamosi ambapo alimtaka Meneja wa shirika hilo kueleza mkakati wa kumaliza tatizo hilo.
“Nimekuja hapa kwakuwa naona sasa tunageuka makubaliano ya kukata umeme kila jumamosi tu, sasa katikati ya wiki umeme unakatika sana, lakini hata hayo makubaliano ya jumamosi naona muda unaenda tu hatujui lini mtakamilisha matengenezo mnayoyafanya kila Jumamosi”, Brig. Jen. (Mst) Mwangela.
Ameongeza kuwa Mkoa unapata athari kubwa kufuatiwa kutokuwepo umeme wa uhakika kwakuwa shughuli za uzalishaji viwandani, shughuli za majumbani zinazohitaji umeme na hata baadhi ya huduma za kijamii zinazohitaji uwepo wa umeme wa uhakika zinaathiriwa huku akielezea kuwa wananchi hawapewi taarifa.
“Nawaelekeza kuanzia sasa mkizima umeme au hata ikitokea hitilafu taarifa na sababu zitolewe ili ifahamike umeme umekatika kwa sababu zipi, tatizo la umeme kwetu limeshakuwa kero kubwa kwani hakuna maendeleo hususani ya viwanda bila umeme”, amesisitiza Brig. Jen. (Mst) Mwangela.
Brig. Jen. (Mst) Mwangela. amewataka TANESCO Songwe waongeze ujuzi na maarifa kutoka kwa maeneo mengine ambao wameweza kutatua matatizo kama hayo pia wafahamu mahitaji ya vifaa vinavyotakiwa kwa ajili ya matengenezo wanayoyafanya.
Naye Kaimu Meneja TANESCO Mkoa wa Songwe Aristidia Clemence amesema kuwa kukatika umeme mara kwa mara kunatokana na Mvua zonazoendelea kunyesha kwani husababisha nguzo kuanguka na pia radi hupasua vikombe katika nguzo.
Amesema matatizo ya Umeme Mkoa wa Songwe yataisha pale ambapo Mradi wa Umeme wa Gridi ya Taifa kutoka Iringa mpaka Nkangamo Momba, wa Kilovoti 400 utakapokamilika kwani kwa sasa umeme unaopatikana ni mdogo na unapatikana kwenye laini moja yenye Zaidi ya Kilometa 1200 tofauti na mikoa mingine yenye line kumi na umeme wa kutosha.
“Hata sisi tunaumia umeme unapokatika kwani tunatambua umuhimu wa umeme na ndio maana tunafanya kazi usiku na Mchana, Mkoa huu ulikuwa na matatizo ya nguzo chakavu pia baadhi ya vikombe vimeharibika ndio maana kila jumamosi tunazima umeme ili kubadilisha nguzo na vikombe hivyo”, ameeleza Clemence.
Clemence ameongeza kuwa kwa sasa kuna ujenzi wa switching station ambao unatarajiwa kukamilika hivi karibuni na kusaidia endapo kuna hitilafu imetokea sehemu moja umeme usikatike mkoa mzima tofauti na sasa ambapo hitilafu ikitoa wilaya moja mkoa mzima unakosa umeme.
“Pia tatizo lililopo sasa ni hitilafu ikitokea mkwajuni Songwe umeme ukikatika ni Mkoa Mzima ila ujenzi huu wa Switching Station utasaidia kuondoa tatizo hilo, pia mradi ule wa Iringa wa Gridi ukikamilika matatizo ya umeme yatakwisha hivyo nawasihi wenye viwanda na wenye nia ya kuwekeza kwenye viwanda wasikate tamaa”, amefafanua Clemence.
Kwa upande wao wananchi Mkoani Songwe wameiomba serikali iwasaidie uwepo wa umeme wa uhakika ili waweze kuzalisha na kufanikisha uchumi wa viwanda, aidha wamesema kukatika kwa umeme mara kwa mara kunaathiri upatikanaji wa huduma za kijamii kama vile baadhi ya huduma za afya hospitalini
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.