USALAMA WA MADEREVA, MALI ZAO UMEIMARISHWA TANZANIA NA ZAMBIA, RC MGUMBA.
SONGWE: Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Omary Mgumba amewaondoa hofu madereva wa maroli juu usalama wao kwa wanaoenda nchi jirani na wanaoingia nchini kupitia mpaka wa Tunduma kutokana na uwepo wa mgomo wa madereva ambao unashinikizwa na baadhi ya madereva.
Mkuu wa Mkoa amewaondoa hofu juu usalama baada ya kutembelea baadhi ya pakingi za maroli ambao walikuwa tayari kuendelea na safari yao ya kwenda nchi jirani na Dar es Salaam lakini walikuwa wanaogopa kutokana na vitisho vya kupigwa mawe kutoka kwa watu wanaojiita kamati ya roho mbaya katika maeneo mbalimbali hapa nchini wakiwa barabarani.
Mkuu wa Mkoa amesema Serikali ya Mkoa kupitia vikao vya ujirani mwema wameongea na Serikali ya Zambia ambao nao wameimarisha ulinzi mara dufu dhidi ya madereva wa maroli wanaopita Zambi.
Pia, Mkuu wa Mkoa amewaonya watu wote wanaojiita kamati ya roho mbaya ambao wanatishia usalama wa raia na mali zao haswa madereva wa maroli kuacha tabia hiyo mara moja kwani sasa Serikali inakwenda kuchukua hatua kali dhidi ya watu hao.
Mkuu wa Mkoa amesema madereva walileta hoja 18 kuwalalamikia wamiliki wao na wamiliki walileta hoja 14 na Serikali ikafanya vikao zaidi ya 6 kati ya madereva na wamiliki kupitia hoja moja baada ya nyingine hoja zote zimepatiwa majibu ikiwemo ya mkataba na kubaki na hoja ya posho ya kwenda nchini Congo ya kurudi Tanzania na Posho ya kukaa siku za ziada hoja ambazo zote Serikali imesimamia na pande zote mbili kusaini makubaliano hayo kati ya viongozi wa madereva, vyama vya madereva, wamiliki na Serikali ikiwa shuhuda ya makubaliano hayo.
“Mfano wa hoja ya posho ya kwenda nchini Congo madereva walikuwa wanataka kulipwa shilingi laki nane lakini wamiliki walikuwa wanataka kulipa shilingi laki sita hoja ambayo pande zote walishindwa kufika muafaka ndipo Serikali ikaingilia kati kwa kujumulisha fedha ya madereva laki nane na laki sita ya wamiliki na kuzigawa kwa mbili na kupata shilingi laki saba ndio yakawa makubaliano ya posho ya kwenda nchini Congo ambayo dereva anapaswa kulipwa” Mhe. Omary Mgumba.
Hoja ya pili ilikuwa ni posho ya kurudi Tanzania kwa dereva akiwa nchini Congo, ambapo madereva walikuwa wanahitaji kiasi cha shilingi laki tatu na elfu hamsini na wamiliki wanahitaji kutoa laki tatu kamili baada ya kushindwa kuelewana, Serikali ikazijumlisha fedha izo na kuzigawa kwa mbili na kupata shilingi laki tatu na elfu thelathini ndio yakawa makubaliano.
Hoja ya tatu, ilikuwa ni posho ya kushusha mzigo nchini Congo madereva walikuwa wanaitaji wapatiwe Dola laki mbili na wamiliki walikuwa wanataka kutoa dola laki moja na nusu baada ya kushindana, Serikali ikachukua na kuzijumlisha zote na kugawa kwa mbili na kupata Dola laki moja na elfu sabini na kuwa makubaliano.
Hoja ya nne, Posho ya siku za ziada (Overstay) kama gari itakaa zaidi ya siku ishirini nje ya nchi madereva walikuwa wanahitaji walipwe Dola 10 kwa siku kuanzia siku ya 21, makubaliano ambayo madereva waliingia na wamiliki wa magari.
Mkuu wa Mkoa amesema makubaliano hayo ni baada ya wamiliki wa maroli, madereva na vyama vya madereva wa maroli kufanya vikao zaidi ya sita na kikao cha karibuni kilifanyika mkoani Songwe katika mpaka wa Tunduma ambacho wamiliki wa maroli, madereva pamoja na vyama vya madereva walikaa kwa pamoja na kukubaliana hoja zote izo na Serikali akiwa mdau wa wote akishuhudia.
Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Omary Mgumba ametoa wito kwa madereva kama wana hoja mpya tofauti na zile walizowasilisha ambazo Serikali imeweza kuzitatua basi wawasilishe kwa maandishi Serikalini ili waweze kuzifanyia kazi kwa haraka kama walivyozitatua hoja nyingine, kwani iko kwa ajili kusimamia maslahi ya pande zote mbili za madreva na wamiliki wa maroli.
“Madereva nyie mnaweza kuona kama ni swala la mshahara tu, lakini Serikali tunaliona ili kama vita ya kiuchumi kwani baada ya Mhe. Samia Suluh Hassan Rais wa Tanzania kufungua nchi kiuchumi wawekezaji wengi wanakuja na bandari ya Dar es Salaam imekuwa ikipokea mizigo mingi sasa wasije kutokea watu wachache miongoni mwenu ambao wakatumika ili washindani wetu kwa bandari ya Dar es Salaam waanze kuona sio njia sahihi kupitishia mizigo yao kutokana na migomo ya mara kwa mara” Mhe. Omary Mgumba.
Baadhi ya madereva wa maroli wameonyesha kutopata taarifa sahihi juu ya hatua ambazo Serikali imechukua dhidi ya hoja zao baada ya Mkuu wa Mkoa kukutana nao na wakauliza hoja zile zile ambazo Serikali ilikaa pamoja na wamiliki wa maroli, vyama vya madereva wa maroli pamoja na madereva kuzipatia ufumbuzi.
Ismail Juma, Dereva wa roli amesema hawajui kama kwenye mgomo huu wanaigomea ni Serikali au matajiri kwa sababu kampuni yao inawapa sitahiki zote ambazo walikubalina kwenye mkataba, hivyo amewashauri madereva wenzao ambao hawana tatizo na matajiri wao waendelee na safari kama kawaida ila kwa wale ambao matajiri wao hawajaelewana basi waendele kupaki gari.
Mgomo wa maroli wa sasa, kama Serikali sio chanzo ila tunachotaka kupata kwa madereva ni kampuni ipi ambayo hadi sasa haitekeleze makubaliano ambayo yalisainiwa na pande zote kati wamiliki, viongozi wa vyma vya madereva na Serikali ili hatua zichukuliwe dhidi kampuni hiyo na sio kuitisha mgomo kwa madereva wote wakati kuna kampuni zinatekeleza makubaliano yote bila shida, amesema Mhe. Omary Mgumba.
Waziri Mkuu wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akiwa Dodoma amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan itahakikisha inaendelea kusimamia madai ya madereva pamoja na haki za waajiri katika kutekeleza madai ya madereva wa maroli.
Waziri Mkuu amesema Serikali haipendi kuona mgogoro huo ukiendelea na kuathiri shughuli za waajiri ambao wametekeleza majukumu yao, hivyo ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani iondoe vikundi vinavyozuia madereva hao kutekeleza majukumu yao. “Sheria zipo wahakikishe zinasimamiwa na hatua zichukuliwe kwa wanaozikiuka.”
Mheshimiwa Majaliwa ametumia fursa hiyo kukitaka Chama Cha Madereva nchini kiruhusu huduma za usafirishaji ziendelee kutolewa wakati Serikali ikiendelea kushughulikia masuala yao. “Serikali haitaridhika kuona madereva wanalalamika kila siku na pia si vizuri waajiri wakabebeshwa mizigo iliyo nje ya sheria.
Makampuni mbalimbali kama vile ya Usangu, ASAS, Meru, GSM yameanza kuendelea na safari zao kama kawaida baada ya kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa kuwatembelea na wameiomba Serikali ya Tanzania kuimarisha ulinzi na usalama wa mali zao na madereva dhidi ya watu wanaojiita kamati ya roho mbaya.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.