Wizara ya Mifugo na uvuvi imewataka Wafugaji wa ng'ombe wilayani Momba mkoani Songwe kuboresha mbegu za mifugo yao kwa kununua mbegu bora za Ng'ombe zitakazo ongeza kipato chao ukilinganisha na sasa ambapo wanafuga ng'ombe wa zamani ambao ni wadogo na bei yake kuwa ndogo sokoni.
Akiongea katika mafunzo yaliyoandaliwa na Wizara ya Mifugo kwa Maafisa mifugo na wafugaji katiaka kata ya Ivuna wilayani Momba Mkoani Songwe Afisa Mifugo Wizara ya Mifugo na Uvuvi idara ya uzalishaji na Masoko Gerald Mtama alisema ili kuongeza uzalishaji na kuinua uchumi wa wafugaji wizara inatoa elimu kwa wafugaji namna ya kuachana na ufugaji wa zamani ambao faida yake ni ndogo kwa kuwa mifugo wanayofuga huuzwa kwa bei ndogo.
Alisema kwa wafugaji wanaofuga mifugo kwa ajili ya nyama kama walivyo wa wafugaji wa Momba wanatakiwa kununua madume ya mbegu bora yaliyoboreshwa aina ya Borani na Mpwapwa yatakayotumika kupanda mifugo ya kienyeji ili kuteketeza kabisa mbegu ya zamani ambayo haina faida kubwa.
Alizitaja baadhi ya sifa za Ng'ombe walioboreshwa kuwa ni pamoja kukua haraka ,kuwa na nyama nyingi pamoja na kuwa na bei nzuri katika soka la ndani na nje ya nchi ambalo litamnufaisha zaidi mfugaji.
"Wafugaji tubadilike hawa ng'ombe wa asili huchelewa kukua, hutoa nyama kidogo baada ya kuchinja na huwa na bei ndogo Sokoni, ng'ombe aliyeboreshwa akipanda wa asili tunapata mifugo bora zaidi kwa sababu ya kuwa na vina saba vingi" alisema Mtama.
Naye mtendaji Mkuu wa Wakala wa Vyuo vya Mafunzo ya Mifugo(LITA) Dk Pius Mwambene alisema kutokana na uchache wa watalaam wa katika sekta ya ufugaji na uvuvi serikali ya awamu ya tano imeamua kujikita katika kuboresha mbegu za mifugo, kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na kupe, kudhibiti mazao yatokanayo na mifugo kuanzisha vyama vya ushirika na kutoa elimu kwa wafugaji na maafisa mifugo.
hivyo amewataka wafugaji kuwa kwenye vikundi vya ushirika ili waweze kunufaika zaidi na ufugaji kwa kufikiwa zaidi na huduma mabalimbali zikiwemo za huduma za chanjo na kuletewa mbegu za ng'ombe walioboreshwa.
Wafugaji waitaka Serikali kuwaletea karibu mbegu za madume yaloboreshwa haraka
Baada ya kupewa elimu ya namna ya kuboresha mifugo yao wafugaji wengi wamehamasika na kuomba serikali kupitia wizara ya mifugo na uvuvi kuwasafirishia na kuwawekea mbegu za ng'ombe walioboreshwa karibu ili waweze kununua na kubadilisha kizazi cha Ng'ombe wakienyeji ambao ni wadogo.
Mfugaji kutoka kata ya Mpapa tarafa ya Kamsamba Chales Manangu alisema wanafuga sana lakini jambo kubwa wanalolikosa ni elimu , hivyo kudai kuwa wapo tayari kubadilisha mifugo walioizoea kwa kununua mbegu bora zilizoboreshwa na serikali ili kupunguza mifugo na kufuga kwa tija .
"Tunaiomba serikali itusogezee mbegu zilizoboreshwa hukuhuku kwetu tuko tayari kununua ili tuboreshe , tuongeze uzalishaji wa mifugo na tutokomeze ufugaji wa mazoea" alisema Manangu.
Naye Gaudence Sichalwe mfugaji na katibu wa wafugaji wilaya ya Momba alisema kuwa wamekuwa wakifuga kwa mazoea siku zote , na kudai kuwa elimu ambayo imeanza kutolewa na wizara ya Mifugo itawabadilisha kwa kuboresha ufugaji wao.
Alisema wanatamani muda mrefu kupata mbegu bora za mifugo lakini namna ya kupata ndio shida hivyo kwa kuwa Momba wanafuga sana wanaitaka serikali kuwaletea mbegu bora za mifugo karibu ili waweze kununua na kubadilisha kizazi cha zamani ambacho hakina faida kubwa kutokana na udogo wa mifugo.
Mkuu wa wilya ya Momba Juma Irando aliitaka Wizara ya Mifugo na uvuvi kuhakikisha mafunzo hayo kuwa endelevu ili kuweza kuwabadilisha wafugaji ambao mara nyingi hupenda kujitenga na kuhama hama kutokana na kukosa elimu ya ufugaji uliobora.
Pia aliwataka wafugaji kutoa ushirikiano wa kutosha kwa serikali yao inayowajali pindi wanapotaka takwimu ya mifugo yao ili waweze kuandaliwa chanjo bora inayoendana na magonjwa mbalimbali ya mifugo kama vile Kimeta, chambavu na kuoza kwato.
Na: Baraka Messa- Mbozi
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.