Wajasiriamali wadogo na wa kati wanaosindika vyakula Mkoani Songwe wamehimizwa kuzingatia ubora na usalama wa bidhaa wanazozalisha ili kulinda afya za wanaotumia bidhaa zao.
Rai hiyo imetolewa mapema leo na Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Songwe Herman Tesha wakati akifungua mafunzo ya siku mbili ya wajasiriamali wanaosindika vyakula mkoani hapa yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA).
Tesha amesema, kuelekea uchumi wa viwanda wasindikaji hao wanapaswa kuzingatia sheria na taratibu pamoja na matumizi ya teknolojia mpya na za kisasa zaidi katika kusindika bidhaa zao ili ziweze kushindana katika soko kitaifa na mataifa.
“Teknolojia inakua na mawasiliano yamerahisishwa, wasindikaji msibweteke hakikisheni bidhaa zenu ni bora ili kwanza muweze kulinda afya za watumiaji pili muweze kushindana na kuliteka soko la kitaifa na kimataifa”, amesisitiza Tesha.
Aidha amewataka wajasiriamali hao kuwa mabalozi wazuri wa elimu waliyoipata kwa wananchi wengine na wajasiriamali wengine kutokana na kuwa mkoa wa Songwe una pakana na nchi jirani na hivyo kuwa na uwezekano wa kupitishwa bidhaa zisizo halali.
“Sisi tuko mpakani, vipodozi haramu na vyakula visivyo faa vinaweza kuzagaa katika maeneo yetu, hivyo basi elimu hii tunayoipata katika mafunzo haya hasa ya kutambua bidhaa halali na bandia itusaidie kuwa mabalozi wazuri pamoja na sisi wenyewe kuhakikisha bidhaa zetu ni halali”, ameongeza.
Tesha amewataka wajasiriamali hao kutosubiri kuletewa mafunzo bali pale wanapoona kuna uhitaji wazifuate taasisi husika ili ziwape elimu hiyo huku akisisitiza kuwa taasisi hizo pia zina wajibu wa kuwasaidia wajasiriamali kwa kuwapa mafunzo na elimu.
Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa Chakula kutoka TFDA Justin Makisi ameeleza kuwa idadi kubwa ya wajasiriamali wamekuwa wakiendesha shughuli zao bila kujua wala kufuata sheria na taratibu.
Makisi ameeleza kuwa wajasiriamali hao hasa wasindikaji wa vyakula wadogo na wa kati hawajasajili bidhaa zao kutokana na kushindwa kumudu gharama za uchunguzi wa maabara wa bidhaa zao ili ziweze kusajiliwa huku wengine wakiwa hawafahamu endapo wanatakiwa kusajili bidhaa zao.
Naye Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt. Kheri Kagya amewataka wajasiriamali hao kufuatilia mafunzo hayo kwa umakini kwakuwa yatawasaidia katika ushindani wa bidhaa zao kwenye soko la kimataifa.
Dkt Kagya amewaeleza wasindikaji hao kuwa ubora na usalama wa bidhaa zao ni kigezo mojawapo katika kuliteka soko la kimataifa na hivyo kukuza uchumi wa taifa.
Kwa upande wao wajasiriamali wasindikaji wa vyakula mkoani Songwe wameeleza kuwa changamoto walizonazo katika utekelezaji wa shughuli zao ni pamoja na majengo ya kusindikia bidhaa zao kutokidhi vigezo vya TFDA pamoja na uhaba wa vifungashio bora vya bidhaa zao.
Wajasiriamali wanaosindika vyakula mkoani Songwe wakishiriki mafunzo ya siku mbili yaliyoandaliwa na Mamlaka ya Chakula na Dawa Nchini (TFDA).
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.