WANANCHI WANUFAIKA NA AJIRA KWENYE MIRADI YA MAJI.
MBOZI: Wananchi waliopata ajira kwenye miradi ya maji inayotekelezwa na Wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mbozi wameishukuru Serikali kwa kuleta miradi ya maji iliyopelekea wapate kazi kwenye miradi hiyo.
Wananchi wameonyesha furaha hiyo wakiwa wanaendelea na kazi katika mradi wa maji wa Old Vwawa ambao uko hatua za ukamilishaji ili uanze kutoa maji safi na salama kwa ajili ya wananchi wapatao elfu 3 wanaoishi Old Vwawa.
Keston Mwashiuya fundi aliyepata kazi ya ujenzi katika mradi wa Old Vwawa amesema ajira zinazotolewa na RUWASA ni nzuri, wanalipa vizuri na ameiomba Serikali kuendelea kuleta miradi ya maji wilaya ya Mbozi ili wazidi kunufaika na kukuza uchumi wa familia zao.
“Sisi wananchi wa hali ya chini miradi hii mbali ya kutuletea maji safi na salama lakini inatusaidia sana kwa kutupatia ajira na maisha yetu yanaendelea vizuri” Keston Mwashiuya.
Elia Nzunda ameiomba RUWASA kuendelea kuwaamini katika kazi mbalimbali na wao watafanya kazi za ubora na thamani kama wanavyohitaji RUWASA kwani kwa takribani miaka 3 nimefanya kazi za ufundi katika miradi mbalimbali inayotekelezwa na RUWASA wilaya ya Mbozi na nimeona tofauti na kazi ambazo alikuwa anafanya sehemu nyingine.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbozi, Mhandisi Gratius Haule amesema kwa makadirio mradi moja wa maji unatoa ajira za mafundi wapatao 20 kwa ujenzi wa nyumba ya pampu na tenki la kuhifadhia maji, wananchi kati ya 100 na 200 wanapata ajira za kuchimba mitaro ya kulaza mabomba za maji na kupelekea mradi moja kuajiri watu zaidi ya 200.
“Naishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa sasa Wilaya ya Mbozi katika mwaka wa fedha 2022/2023 Serikali inampango wa kujenga miradi 6 kwa shilingi Bilioni 5 kwenye vijiji mbalimbali ambavyo havina huduma ya maji safi na salama, tunategemea tutazalisha ajira nyingine nyingi katika miradi hii” Mhandisi Gratius Haule.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Mbozi, Mhandisi Gratius Haule amesema Serikali ya awamu ya sita chini ya Mhe. Samia Suluh Hassan Rais wa Tanzania imepanga ifikapo 2025 vijiji vyote ndani ya wilaya ya Mbozi viwe na maji safi na salama na ujenzi wa miradi utaendelea kila mwaka.
Wakati RUWASA inaanzishwa 2019 upatikanaji wa maji katika wilaya ya Mbozi ulikuwa asilimia 46 lakini hadi 2022 upatikanaji wa maji kwa sasa umeongezeka na kufika asilimia 73 zote izi juhudi kubwa ambazo zimefanywa na Serikali, lengo ifikapo 2025 maji vijijini yapatikane kwa zaidi ya asilimia 100.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.