Wanawake Mkoani Songwe wameaswa kutonyamazia vitendo vya rushwa ya ngono ili waweze kujikomboa kifikra, kiuchumi na kisiasa katika harakati za kufikia usawa wa kijinsia kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Akisoma hotuba ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig Jen. (Mst) Nicodemus Mwangela katika maadhimisho ya siku ya wanawake Duniani yaliyofanyika Kimkoa Wilayani Ileje, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi John Palingo amesema rushwa ya ngono inapaswa ithibitiwe kwa nguvu zote
“Nawasihi sana wanawake wanaokumbana na udhalilishaji huu wa kuombwa rushwa ya ngono watoe taarifa katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) pia wananchi wengine watoe taarifa mara tu wanapokutana na matatizo ya rushwa ili taasisi husika ziweze kushughulikia”, amesema Palingo
Ameongeza kwa kuziagiza halmashauri za Mkoa wa Songwe kuhakikisha zinaendelea kupiga vita unayanyasi na ukatili wa kijinsia, taasisi zote zinazohusika na mapambano hayo ikiwa ni pamoja na dawati la jinsia kuwachukulia hatua wote wanaofanya vitendo hivyo.
Palingo ameelekeza kuwa halmashauri ziweke mazingira mazuri ya masoko ya bidhaa na mazao yanayozalishwa na wanawake, kutenga fedha kwaajili ya kuwawezesha wanawake kuwa na uwezo wa kumiliki viwanda na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake.
Akisoma risala kwa niaba ya wanawake Afisa Maendeleo ya Jamii Roida Kyomo amesema wanawake wamekuwa wakizalisha kidogo kutokana na ukosefu wa masoko, elimu na mitaji wakti uwezo wa kuzalisha bidhaa na mazao mengi wanayo.
Kyomo ameongeza kuwa uwepo wa mashauri 442 ya unyanyasaji wa kijinsia unaonyesha kuwa tatizo hilo bado lipo hivyo ameiomba serikali kuendelea kuhamasisha jamii kuachana na mila kandamizi kwa wanawake ili muda unaotumika katika kusuluhisha matatizo hayo utumike katika kuzalisha mali ili kukuza uchumi.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.