Kuelekea Tanzania ya Viwanda wanawake hususani wa Mkoa wa Songwe wameelezwa kuwa wanayo fursa kubwa katika kuanzisha viwanda vipya na kusaidia kufufua viwanda vilivyopo kwa kupeleka bidhaa zao katika viwanda hivyo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa ameeleza hayo mapema leo katika viwanja vya shule ya Msingi Tunduma katika maadhimisho ya Siku ya wanawake Duniani huku akisisitiza kuwa wanawake sasa wajikite katika kuanzisha viwanda.
“Mwanamke amekuwa mzalishaji mkubwa wa mazao ya shambani, ameweza kuongeza thamani ya mazao yake pamoja na shughuli nyingine za uzalishaji mali, tunapoelekea kwenye uchumi wa viwanda hii ni fursa kubwa kwakuwa sasa tunatakiwa kuanzisha viwanda na tayari malighafi tunazo za kutosha”, amesema Gallawa.
Ameongeza kuwa wanawake wanapoendelea kuzalisha mali wajikite sasa katika kuboresha bidhaa zao ili ziweze kupata soko na kukubalika katika viwanda na masoko pamoja na kujiunga kwenye vikundi ili kupata urahisi wa mikopo.
Aidha Gallawa ameziagiza halmashauri zote Mkoani Songwe kuhakikisha wanatoa mikopo kwa vikundi vya wanawake, ambayo itawasaidia kununua mashine na malighafi kwa ajili ya kuanzisha kiwanda huku akisisitiza mkopo kwa kikundi kimoja usipungue shilingi milioni 20.
“Kwa mkoa mzima wa Songwe tulitenga bilioni 1.2 kwa ajili ya wanawake, vijana na walemavu sasa naagiza halmashauri zote hakikisheni mnavipa vikundi vyenu mikopo, angalau isipungue milioni 20 na sio kuwapa fedha kidogo ambazo haziwanui kiuchumi’’, amesisitiza Gallawa.
Gallawa amezitaka halmashauri kusimamia vikundi hivyo kwa kuwatoa wataalamu kama maafisa biashara, vijana, ushirika na maendeleo ya jamii ili kuviandalia vikundi maandiko ya miradi yao na ushauri wa kitaalamu wa uendeshaji wa vikundi vyao.
“Jukumu la halmashauri ni kulea vikundi vyote, sio mkiwapa mkopo mnawatelekeza, mnatakiwa kuvisaidia kuandaa andiko la mradi, hii sio huruma au hisani ni wajibu wenu”, amefafanua Gallawa.
Gallawa amewasihi pia wanawake kugombea nafasi za uongozi kuanzia ngazi ya serikali za vijiji ili wawe watetezi wa wanawake akitoa mfano kuwa kati ya vijiji 307 vya mkoa wa Songwe ni kijiji kimoja tu ndio kuna mwenyekiti wa kijiji mwanamke.
Nao wanawake waliojitokeza katika maadhimisho hayo wamemueleza Mkuu wa Mkoa changamoto za kukosa mikopo na elimu zaidi ya ujasiriamali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Mwanamke mkazi wa Tunduma akionyesha kuwa wanawake wanaweza kufanya kazi yoyote kwa kumsaidia fundi aliyekuwa akijenga katika kituo cha afya cha Tunduma.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa akizungumza na mgonjwa katika kituo cha afya Tunduma alipowatembelea wagonjwa na kuwafariji kama sehemu ya maadhimisho ya siku ya wanawake duniani mapema leo.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.