Naibu Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mhe. Deogratius Ndejembi amewaasa wanufaika wa mfuko wa jamii wa kuwezesha kaya masikini (TASAF) kutozitumia fedha wanazopata katika anasa, badala yake wazitumie kuanzisha miradi midogo itakayowaondoa katika hali waliyo nayo.
Kauli hiyo ameitoa jana kwa nyakati tofauti alipokuwa anazungumza na wakazi wa vijiji vya Msangano, Nkala na Nkangamo wilayani Momba mkoani Songwe kuwa Serikali inatoa fedha hizo kwa lengo la kuzijengea uwezo kaya masikini ili ziweze kupiga hatua mbele na kuanza kujitegemea na kumudu kugharamia huduma muhimu za kila siku.
Alisema mradi huo utumike kama yalivyo malengo yake ya kuwatoa katika hali duni na kupata nafuu na kwamba hautakuwa wa kudumu hivyo walengwa wanapaswa kuzitumia vizuri fedha hizo.
"Tunataka kuona kama mnufaika alikuwa hali milo mitatu kwa siku baada ya mradi awe anakula, kama watoto walikuwa hawaendi shule wawe wana kwenda shule, kama hakuwa na mbuzi apate na hata makazi bora ikiwezekana kwakuwa fedha hizi sio za milele zina mwisho wake" alisema Naibu Waziri Ndejembi
Aidha aliongeza kuwa wakati mpango wa TASAF awamu ya tatu mzunguko wa pili unaotarajia kuanza Julai, vijiji ambavyo havikunufaika vitaingizwa ili navyo vinufaike na kuonya wale wanaoshawishi wengine wasijitokeze kwenye mchakato wa kubaini wanufaika unaofanyika katika vijiji.
Naye Mbunge wa Momba Condesta Sichalwe aliwataka wakazi wa eneo hilo kuendelea kuiunga mkono Serikali yao sikivu na kuwa changamoto mbalimbali zinazowakabili zinafanyiwa kazi.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.