Katika kutekeleza maagizo ya serikali ya kuhakikisha wasafiri wote wanaotoka katika nchi zenye maambukizi Zaidi ya Virusi vya Corona wanatengwa, jumla ya wasafiri 84 kutoka Nchi ya Afrika Kusini wamewekwa karantini kwa muda wa siku 14 Katika halmashauri ya Mji wa Tunduma.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela ameyasema hayo alipofanya ukaguzi wa maandalizi ya utayari wa kupambana na Ugonjwa wa Virusi vya Corona kwa Mkoa wa Songwe hususani maeneo ya Mipakani yaani katika Halmashauri ya Wilaya ya Ileje na Halmashauri ya Mji wa Tunduma.
Brig. Jen. Mwangela amesema wasafiri hao ambao ni watanzania 55 na raia wengine kutoka Congo, Afrika Kusini, Kenya na Uganda walipoingia nchini kupitia mpaka wa Tunduma walipimwa na kukutwa hawana dalili za virusi vya Corona na kwakuwa wametoka katika nchi yenye maambukizi Zaidi wametengwa katika karantini.
Amesema utaratibu huo ni kwaajili ya kuwaaangalia ndani ya siku 14 kama watakuwa hawana dalili za Ugonjwa wa Virusi vya Corona wataruhusiwa kuendelea na safari zao.
Brig. Jen. Mwangela amewaagiza viongozi katika sekta mbalimbali kuendelea kutoa elimu ya namna ya kujikinga na Virusi vya Corona pia katika ofisi na taasisi zote usafi uzingatiwe huku suala la kunawa mikono kwa maji na sabuni liwekwe kipaumbele kila mahali.
Aidha ameliagiza jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kufanya msako katika maeneno ya stendi za mabasi endapo kutakuwa na raia kutoka katika nchi zenye maambukizi Zaidi ya Virusi vya Corona na wamepitia njia zisizo rasmi waweze kuwekwa karantini.
Naye Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe George Kyando amesema jeshi hilo limepiga marufuku kwa mabasi kujaza abiria kuliko uwezo wa gari, kutokuwa na vitakasa mikono kwenye mabasi au maji na sabuni kwa ajili ya kunawa na marufuku ya mabasi kuanza safari bila kupuliziwa dawa.
Amesema yeyote atakayepuuzia marufuku hizo ambazo zimelenga kuweka tahadhari ya kutosambaza ugonjwa wa Virusi vya Corona atakuwa anataka kusambaza ugonjwa kwa makusudi jambo ambalo ni kosa kisheria hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.
Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma Dkt Enock Mwambalaswa amesema wasafiri wote waliowekwa karantini wanapimwa mara mbili kwa siku ili kufuatilia maendeleo ya afya zao na endapo atatokea mwenye dalili za Virusi vya Corona hatua za haraka zitachukuliwa lakini hadi sasa wote wanaendelea vizuri na hakuna aliyebainika kuwa na viashiria vya ugonjwa huo.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.