Takribani Wasichana 20,900 wenye umri wa miaka 14 wanatarajia kupata chanjo ya kuwakinga dhidi ya ugonjwa wa saratani ya Mlango wa kizazi Mkoani Songwe kuanzia Aprili 23 Mwaka huu.
Chanjo hiyo inatolewa kwa wasichana wenye umri wa miaka 14 kwa mara ya kwanza na dozi ya pili watapewa miezi sita baadaye ili kukamilisha kinga dhidi ya saratani hiyo.
Akizindua chanjo hiyo katika shule ya Sekondari ya Vwawa Wilaya ya Mbozi Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa amesema chanjo hiyo ni juhudi za serikali za kuboresha na kuokoa maisha ya wananchi hasa kwa magonjwa yanayozuilika.
Gallawa ameeleza kuwa chanjo hiyo ni salama na imethibishwa na shirika la Afya duniani na Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania hivyo wazazi na walezi washirikiane na serikali kuhakikisha wasichana hao wanapata kinga hiyo.
“Kinga ni bora kuliko tiba, tukishirikiana vyema wazazi na serikali tutaweza kuokoa maisha ya mabinti zetu, ugonjwa huo wa saratani ya mlango wa kizazi inaongoza kwa vifo vya akina mama vitokanavyo na saratani nchini kwetu”, amesisitiza.
Aidha amewasihi wasichana wote kutoshiriki vitendo vya ngono katika umri mdogo kwakuwa ni moja ya chanzo kinachoweza kusababisha saratani ya mlango wa kizazi pamoja ikiwa ni pamoja na kutojiingiza katika uvutaji wa sigara.
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Kheri Kagya amesema chanjo hii inatolewa bure katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya na katika huduma za mkoba kwenye shule mbalimbali.
Dkt. Kagya ameongeza kuwa chanjo hii itakuwa endelevu huku akibainisha kuwa takwimu zinaonyesha kila mwaka akina mama elfu 50 wanapata saratani hii na asilimia 58 ya wanaopata ugonjwa huo hufariki.
Naye Atuganile Shimwela mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya Sekondari ya Vwawa ameeleza kuwa amefurahi kupatiwa chanjo ya kumkinga dhidi ya saratani ya mlango wa kizazi.
“Nimefurahi kwakuwa sasa niko salama dhidi ya saratani hiyo na nitawashauri wenzangu pia wapate chanjo hiyo, pia tutafuata ushauri wa mkuu wetu wa mkoa wa kutojiingiza katika ngono katika umri wetu mdogo ili tuispate magonjwa”, ameeleza. .
Wanafunzi wa Sekondari ya Vwawa Wilaya ya Mbozi wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa wakati wa uzinduzi wa Chanjo ya Saratani ya Mlango wa Kizazi mapema jana.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.