WATOTO 287,512 KUPATIWA CHANJO YA POLIO
SONGWE: Serikali mkoani Songwe imedhamilia kuwafikia watoto 287,512 wenye umri chini ya miaka 5 na kuwapatia chanjo ya matone dhidi ya ugonjwa wa Polio katika kampeni itakayofanyika kwa siku Nne kuanzia tarehe 1 mpaka tarehe 4 mwezi Septemba.
Hayo amesema mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Songwe Mhe. Cosmas Nshenye ambaye ni mkuu wa wilaya ya Mbozi katika kikao cha afya ya msingi ngazi ya Mkoa kilichofanyika leo Agosti 30 na kujadili mikakati ya utekelezaji wa Kampeni ya Polio.
Mhe. Cosmas Nshenye amesema kampeni hii ya Polio watalamu watapita nyumba kwa nyumba na maeneo yote yenye watoto wenye umri chini ya miaka mitano pamoja na vituo vya kutolea huduma za Afya ili kufikia malengo ya kuwakinga watoto wote dhidi ya ugonjwa hatari wa Polio.
Muwakilishi wa Mkuu wa Mkoa, Mhe. Cosmas Nshenye ametoa wito kwa wazazi/walezi wenye watoto wa umri chini ya miaka 5 kuhakikisha mtoto anapata chanjo ya matone ya Polio kwani Mtoto asiyepata chanjo Ni hatari kwa maisha yake na kwa jamii inayomzunguka.
Mwakilishi wa Shirika la Afya Duniani Dkt. Robert Hongo amesema kwa sasa Tanzania haina ugonjwa huu ila inachukua hatua usiingie nchini tangu utangazwe mwezi Januari 2022 nchini Malawi na Msumbuji ambazo ziko jirani na Tanzania na ukizingatia mwingiliano wa watu ni mkubwa hivyo hatua stahili za kuwakinga watoto kwa chanjo ya matone ya Polio ni muhimu.
Katibu Tawala Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda amesema ni vyema jamii ikajua athari za ungonjwa Polio kwa upana wake ili waweze kujitokeza kwa wingi kuwapatia chanjo watoto wao.
"Baada ya Nchi kutoa chanjo ugonjwa huu ulipotea sasa watu wengi wanausikia tu, ni vyema jamii ikapata athari za ugonjwaa huu kwa undani" Bi. Happiness Seneda.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Dkt. Boniface Kasululu amesema katika Kampeni hii ya chanjo ya Polio inayoanza tarehe 1 Septemba watoto wote wenye umri chini ya miaka mitano watapata chanjo hata kama ametoka kupata chanjo hiyo siku moja kabla.
Pia, Dkt. Kasululu amesema ata kama Mtoto alipata chanjo ya matone kwa ratiba yake ya kliniki lakini ndani ya siku nne za kampeni hii Mtoto huyo atapata chanjo tena.
Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Songwe, Bwn. Moses Lyimo amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha kampeni inafanyika vizuri na kuwafikia watoto lengwa wote pamoja na kutoa elimu kwa wazazi/walezi kupitia vyombo vya Habari juu ya athari ya ugonjwa wa Polio kwenye jamii.
Kampeni hii ya Polio ni ya nne tangu kutangazwa kwa ugonjwa wa Polio Nchini Malawi lengo kuchukua hatua ya kujikinga dhidi ya ugonjwa huu hatari wa Polio.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.