Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu amefanya ziara ya siku mbili Mkoani Songwe katika Wilaya za Mbozi na Ileje na kuridhishwa na mafanikio ya sekta ya Afya Mkoani hapa.
Waziri Ummy ambaye amehitimisha ziara yake leo amesema Songwe inafanya vizuri katika sekta ya afya licha ya kuwa na upungufu wa watumishi na baadhi ya miundombinu.
“Songwe mna upungufu wa watumishi takriban asilimia sitini lakini mmefanya vizuri, hii inaonyesha jinsi ambavyo watumishi wa sekta ya afya mkoani hapa wanajitoa kuihudumia jamii”, amesema.
Ameongeza kuwa Songwe imeweza kupunguza vifo vya akina mama wajawazito huku asilimia ya akina mama wanaojifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya ikiongezeka, hii ni ishara tosha kuwa huduma za afya sasa zimeboreka.
“Nimeona kwa mfano Wilaya ya Mbozi kati ya akina mama 12995 waliojfungua sita tu ndio waliopotea maisha, mmejitahidi sana na hongereni pia natamani mikoa mingine ijifunze Songwe hasa katika matumizi ya njia za kisasa za uzazi wa mpango ambavyo zinaweza kupunguza vifo vya akina mama wajawazito”, amefafanua Waziri Ummy.
Ameeleza kuwa Wizara ya Afya itatangaza ajira hivi karibuni na kuahidi kuwa Songwe itapatiwa watumishi kwakuwa iko kati ya mikoa tisa itakayopewa kipaumbele huku akiwataka wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kujiandaa kuwapokea watumishi hao ili waweze kubaki katika vituo walivyopangiwa.
Aidha katika ziara yake Wilayani Ileje katika kata ya Lubanda Waziri Ummy aliweza kushuhudia adha ya miundombinu ya barabara kutopitika kwa urahisi na kuishauri Wakala wa Barabara za Vijijini (TARURA) kushughulikia barabara hiyo ili ipitike kwa urahisi na hivyo kuokoa maisha ya akina mama wajawazito na wagonjwa wengine.
Nao akina mama waliojitokeza katika zahanati ya Lubanda wamemshukuru Waziri Ummy na serikali ya awamu ya tano kwa kuwapatia milioni mia tano zitakazowezesha ujenzi wa chumba cha upasuaji, maabara ya damu, nyumba ya daktari na chumba cha kuhifadhia maiti.
Akina mama hao wamesema adha kubwa waliyokuwa wakiipata hasa ya kusafiri umbali mrefu kwa ajili ya kupata huduma za upasuaji wa mama na mtoto sasa zitakwisha.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Chiku Gallawa amemuhakikishia Waziri Ummy kuwa Mkoa utaendelea kusimamia na kutekeleza kwa ufanisi shughuli na maelekezo yote ya serikali yanayohusu Sekta ya afya ili kuiboresha zaidi sekta hiyo.
Wanakijiji cha Mtura Kata ya Lubanda Wilayani Ileje wakizungumza na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu alipofanya ziara kijijini hapo kujionea maendeleo ya ujenzi katika kituo cha Afya cha Lubanda.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.