WITO WATOLEWA WANAWAKE KUCHANGAMKIA FURSA ZA KIUCHUMI ZILIZOPO.
Wito watolewa kwa Wanawake wa Mkoa wa Songwe kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo katika maeneo yao ili wajiinue kiuchumi na kuondokana na ukatili ambao wamekuwa wakifanyiwa kutokana na kukosa nguvu ya uchumi.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Songwe, Bi. Happiness Seneda wakati wa Kongamano la Wanawake ambalo limefanyika Machi 6 ikiwa ni kuelekea kilele cha siku ya wanawake Duniani Machi 8 ambalo kwa Mkoa wa Songwe litafanyika Wilaya ya Mbozi.
Bi. Happiness Seneda ametoa wito kwa wanawake kujitahidi kujiinua kiuchumi kwasababu wanawake waliowengi wanafanyiwa vitendo vya ukatili kutokana na kukosa nguvu ya kiuchumi na kumtegemea mwanaume tu.
Wanawake tuchangamkie fursa ya mikopo ya 10% ambayo inatolewa kwenye kila Halmashauri kwani fedha zipo na kwa mwaka wa fedha uliopita Halmashauri zimeweza kutoa zaidi ya Bilioni 1.2 ya 10% za mapato ya ndani hii yote ni fursa kwa wanawake, amesisitiza, Katibu Tawala, Bi. Happiness Seneda.
"Wanawake tujitahidi kuimarisha uchumi wetu uwe imara, kwani ukiwa na uchumi imara huwezi kufanyiwa ukatili, hivyo tuchangamkie fursa zilizopo kwenye maeneo yetu" Bi. Happiness Seneda.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Esther Mahawe ametoa wito kwa wanawake kuwa wajasili, kujianini na kuthubutu katika kuanzisha Biashara mbalimbali za kujikomboa kiuchumi.
Mhe. Esther Mahawe amewasihi wanawake kuachana na kauli ya "wanawake wakiwezeshwa wanaweza" badala yake wachangamkie wao fursa mbalimbali za ufugaji, Kilimo na Biashara ili wawe na nguvu ya kiuchumi.
Mfano kwa sasa ni Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan katika uongozi wake amefanya mambo makubwa kiasi cha wanaume nao wanashangaa ambayo yanaonyesha kwa dhati kuwa mwanamke anaweza bila kuwezeshwa.
"Hakuna kilichosimama miradi mikubwa inaendelea, miradi mikubwa inaanzishwa, watoto wetu sasa wanasoma bila ada kuanzia awali hadi kidato cha sita, miundombinu inaboreshwa na wazazi saizi inapofika Januari hawakimbizani na ada" Mhe. Esther Mahawe.
Mhe. Mahawe ametoa wito kwa wanawake kuachana na tabia ya kusubiria Baba alete kila kitu nyumbani kwani izo enzi sasa zimepita enzi za sasa ni Baba na Mama wote wanaleta nyumbani.
Wanawake msiogope kuanguka kwenye Biashara ata ukianguka mara mia inuka anza tena, ni bora uanze ufeli lakini ukiogopa kuanza huwezi kufanikiwa, amesisitiza Mhe. Mahawe.
Wakati huo huo, Katibu Tawala, Bi. Happiness Seneda ametoa wito kwa wanawake kuhakikisha wanawatunza watoto wao dhidi wa watu wenye nia ovu ya kuwafanyia ukatili wakati wanapambana na kutafuta fursa za kiuchumi.
MWISHO.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.