Wizara ya Kilimo imeanzisha Mpango wa kutumia Vijana katika kuendeleza sekta ya Kilimo Nchini kwakuwa wao ni nguvu kazi ambayo inaweza kuleta mabadiliko ya haraka.
Waziri wa Kilimo Japhet Hasunga ameyasema hayo mapema leo wakati akizindua Kongamano la Vijana katika Kilimo lililozinduliwa kitaifa Mkoani Songwe na kushirikisha Vijana kutoka Mikoa ya Songwe, Mbeya, Rukwa na Katavi.
“Wizara ilifanya tathmini na kuona kuwa licha ya mambo mazuri tunayofanya, inabidi katika mikakati yetu tuwe na Mkakati wa Kuwatumia Vijana ili waingie katika Kilimo.”, amesema Waziri Hasunga.
Ameongeza kuwa ili kufanikisha Mpango huo Wizara ya Kilimo itahakikisha ardhi inayofaa kwa Kilimo inapatikana na Kutengwa kwa kuwa na sheria ya kutenga ardhi ya Kilimo, pia Mikoa inapaswa kutenga maeneo yanayo faa kwa ajili ya Kilimo.
Waziri Hasunga amesema Wizara pia itahakikisha upatikanaji wa rasilimali fedha, pembejeo na zana za Kilimo, Miundombinu ya Umwagiliaji inawekwa kwakuwa Mvua ikizidi au kupungua ni hasara kwa Mkulima pamoja na kufundisha mbinu na ujuzi wa ujasiriamali katika kilimo kupitia Makongamano.
Amesema Wizara inatambua kuwa Vijana ndio nguvu kazi huku takwimu zikionyesha kuwa asilimia 96 ya watanzania hawaja ajira hivyo, hiyo ni nguvu kazi ambayo inatakiwa ielekezwe katika Kilimo.
Waziri Hasunga ameongeza kuwa Wizara ina tambua changamoto zilizopo katika sekta ya Kilimo na tayari imechukua hatua kadhaa ikiwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa kusajili wakulima ili watambulike kwa urahisi, kusajili waadau wa Kilimo na Kuanzisha Bima ya Mazao.
Aidha amewataka vijana wote kubadili mtazamo kuwa kilimo ni kushika jembe la Mkono kwakuwa Kilimo ni sekta pana inayojumuisha kulima, kusindika na kuongeza thamani ya mazao, masoko, uhifadhi na pembejeo hivyo wasiache kujikita hata katika moja ya fursa hizo.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amesema Mkoa wa Songwe ni moja kati ya wazalishaji wakubwa wa Chakula Nchini ambapo uzalishaji unafanyika ajili ya Chakula na Kuuza ndani na nje ya nchi pia uhakika wa kuvuna kwa wingi chakula mwaka huu ni mkubwa.
Brig. Jen. Mwangela amesema Mkoa una Hekta Milioni mbili ambapo zinazotumika katika Kilimo ni asilimia 30 tu huku eneo lingine likitumika katika makazi na Misitu lakini eneo kubwa linalobaki halijatumika bado.
Ameongeza kuwa Mkoa una eneo la hekta elfu 18 linalofaa kwa ajli ya kilimo cha Umwagiliaji na pia amewahakikishia vijana kuwa ardhi kwa ajili ya Kilimo Mkoa wa Songwe sio tatizo.
Brig. Jen. Mwangela amesema vijana wabadilike kifikra na kuanza kuthamini kilimo kwakuwa ili kupambana na umasikini vitendo vinahitajika Zaidi kuliko maneno tu ya kulalamika.
Naye Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe Eliniko Mkola amesema vijana wa Kitanzania waliopata mafunzo ya Kilimo Nchini Israel wasikae na elimu hiyo bali wawaelimishe vijana wenzao na mashamba yao yatumike kama madarasa ya kujifunzia Kilimo.
Mkurugenzi wa SUGEC Revocatus Kimario amesema taasisi yake inajihusisha na kuwasaidia vijana katika Sekta ya Kilimo na moja ya changamoto ni mtamzamo wa vijana juu ya kilimo.
Kimario amesema walimu pia wamechangia kutengeneza mtazamo hasi juu ya kilimo kwa kuwa wamekuwa wakitoa adhabu zinazohusiana na Kilimo pale ambapo mwanafunzi anafanya makossa.
“Vijana hawapendi kilimo kwakuwa wamezoe kulima kama adhabu wanapokuwa shuleni, unataka akimaliza masomo akafanye kitu ambacho amekijenga kuwa ni adhabu?, Kilimo ni ajira hivyo waalimu wanapaswa kuacha kukitumia kama adhabu kwa wanafunzi.”, amesema Kimario.
Katibu wa Umoja wa Vijana wa CCM Mkoa wa Songwe Hassan Lyamba ameipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuandaa Kongamano hilo kwakuwa litawafungua akili vijana juu ya fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya Kilimo.
Lyamba ameongeza kwa kuwataka vijana kuhakikisha wanatekeleza kwa vitendo yale yote waliyo jifunza katika kongamano hilo ili wawe sehemu ya mabadiliko katika sekta ya Kilimo nchini.
Kauli Mbiu ya Kongamano la Vijana ambalo linatarajiwa kufanyika nchini Kote katika Kanda Saba ni; “Vijana, Kilimo ni Ajira”.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.