YALIYOJIRI KATIKA ZIARA YA MAKAMU WA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA MHE SAMIA SULUHU HASSAN TAREHE 22 JULAI 2018 WILAYA YA MBOZI
Posted on: July 22nd, 2018
Kituo cha Afya Nanyala kilichozinduliwa na Mhe Samia Suluhu Hassan kimejengwa kwa gharama ya zaidi ya milioni 800 zilizotolewa na kanisa la Uinjilist Tanzania, halmashauri ya Mbozi imetoa milioni 25.6 kwa ajili ya vifaa tiba na wananchi wamejitolea ardhi- Mganga Mfawidhi kituo cha Afya cha Nanyala, Dkt David Mndalla
Ujenzi katika kituo cha Afya Nanyala umehusisha chumba cha upasuaji, wodi ya wazazi, vyumba vya wagonjwa wa nje, wodi mbili za watoto na akina akina mama waliojifungua, jengo la maabara na wodi tatu za wagonjwa- Mganga Mfawidhi kituo cha Afya cha Nanyala, Dkt David Mndalla
Kituo cha Afya Nanyala kitahudumia takribani Wananchi 10,741 kutoka katika vijiji vitano vya Nanyala, Senjele, Songwe, Namlomba, Sumbo na maeneno ya jirani, serikali itatimiza azma ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwakuwa huduma za dharura za uzazi zimesogezwa karibu badala ya kuzifuata mbali kama ilivyokuwa awali- Mganga Mfawidhi kituo cha Afya cha Nanyala, Dkt David Mndalla
Serikali imewapangia watumishi wapya saba katika kituo cha Afya Nanyala ambao ni daktari, wauguzi wawili, tabibu, afisa mazingira na wataalamu wa maabara wawili - Mganga Mfawidhi kituo cha Afya cha Nanyala, Dkt David Mndalla
Nawapongeza kwa kupata kituo cha Afya, awali mlikuwa na zahanati, kituo hiki kimejengwa na kanisa lakini baada ya kukamilika kituo hiki ni mali ya wananchi, jukumu lenu kubwa ni kukilinda na kukitunza -Mhe Samia Suluhu Hassan
Serikali inaushukuru sana uongozi wa Kanisa la Uinjilisti Tanzania kwa ujenzi wa kituo cha Afya cha Nanyala lakini pia wananchi mtoe ushirikiano ili kituo cha Afya kiweze kuendeshwa vizuri- Mhe Samia Suluhu Hassan
Nawapongeza kwa kufanya vizuri kwenye bima ya Afya kwa kuwa na asilimia 77 kwa mkoa wa Songwe, wananchi wote muendelee kujiunga katika bima ya Afya ili muweze kupata huduma zinazotakiwa- Mhe Samia Suluhu Hassan
Serikali imeleta shilingi Bilioni 1.5 kwa ajili ya Hospitali ya wilaya ya Songwe na shilingi bilioni 3.5 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya afya nane ili kuboresha miundombinu na huduma katika sekta ya afya-Mhe Samia Suluhu Hassan.
kujenga miundombinu ni jambo moja na kujikinga ili tusipate madhara ya magonjwa ni jambo lingine, nawasisitiza tujikinge na maabukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU), tuhakikishe watoto na akina mama wajawazito kupata chanjo mdhidi ya magonjwa mbalimbali pamoja na kukata bima ya afya ili kuwa na uhakika wa Matibabu-Mhe Samia Suluhu Hassan
Nawapongeza wananchi kwa kujitolea katika masuala ya kielimu, mkoa wa Songwe kielimu mnafanya vizuri, asilimia 92.5 ya wananfunzi wameripoti shule walizopangiwa kidato cha kwanza hata hivyo Mbozi bado kuna upungufu wa madarasa naomba muendelee na jitihada za kulitatua hilo- Mhe Samia Suluhu Hassan
Mhe Rais anatoa uzito mkubwa kwenye suala la maji na pia sekta hii inahitaji rasilimali nyingi tunakwenda taratibu ila tutafika-Mhe Samia Suluhu Hassan
Ninasikita kuona wananchi wanakata miti ovyo pia wananchi wanajenga kuelekea katika milima, tunaharibu mazingira hivyo ninawashauri tuache kukata miti, tupande miti, na kila mkoa umewekewa lengo la kupanda miti milioni 1.5 kila mwaka hakikisheni mnafanya hivyo- Mhe Samia Suluhu Hassan
Kamati za ulinzi na Usalama za Wilaya na Mkoa zifanye ukaguzi kubaini wanaojenga juu ya milima pamoja na wanaoharibu vyanzo vya maji, vyanzo vya maji vikiharibiwa tutakosa maji hata hiyo miradi ya ujenzi wa matenki ya maji yatakosa maji- Mhe Samia Suluhu Hassan.
Mkoa ufanye ufuatiliaji endapo fedha zilizotolewa na serikali kwa wananchi kupitia mpango wa kunusuru kaya maskini (TASAF) zimewasaidia kujinusuru na umasikini kwakuwa hilo ndio lilikuwa lengo la serikali, wananchi wasizitumie vibaya fedha hizo-Mhe Samia Suluhu Hassan.