Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli ameanza ziara ya siku mbili katika Mkoa wa Songwe ambapo ameonyesha kuridhishwa na kasi ya maendeleo katika Mkoa huu licha ya kuwa umeanzishwa miaka mitatu iliyopita.
Rais Dkt John Pombe Magufuli mara baada ya kuanza ziara yake amezuiliwa na umati wa wananchi katika vijiji vya Nanyala, Mahenje na Mlowo ambapo amewasalimia, amesikiliza na kutatua kero mbalimbali.
Rais Dkt John Pombe Magufuli ameagiza wananchi wa Kijiji cha Nanyala waendelee kufanya shughuli za Kilimo katika eneo la ekari 2,115 linalogombewa kati ya kijiji na kiwanda cha Saruji cha Mbeya, aidha ameelekeza mawaziri husika kujadili namna ya kufuta kesi za wanakijiji 23 za mgogoro huo
Aidha ameelekeza shilingi bilioni 2 zilizobaki katika ujenzi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Songwe zitumike katika kukamilisha ujenzi wa maboma ya vyumba vya madarasa zaidi ya elfu moja yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi.
Rais Dkt John Pombe Magufuli pia ameagiza hekari 50 kati ya 200 katika kituo cha Utafiti wa Kahawa (TACRI) Wilaya ya Mbozi zitumike katika kujenga soko la kisasa la mazao pamoja na stendi ya Mkoa wa Songwe na agizo hili lianze kutekelezwa ndani ya Wiki moja.
Rais Dkt John Pombe Magufuli ameweka jiwe la Msingi katika mradi wa maji wa Mantengu na kuongeza kiasi cha Shilingi milioni 100 katika Mradi huo ili mradi huo ukamilishwe na kuboreshwa ili kuwezesha kutoa maji lita milioni tatu badala ya moja za sasa.
Wakati huo huo Rais Dkt John Pombe Magufuli amezindua kiwanda cha Kahawa cha GDM chenye uwezo wa kukoboa kahawa tani 10 kwa saa na kina thamani ya shilingi bilioni saba huku akimuagiza Waziri mwenye dhamana kuhakikisha barabara ya kuelekea katika kiwanda hicho inajengwa kwa kiwango cha lami.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amemuomba Rais Dkt John Pombe Magufuli awezeshe Mkoa huu kuwa na chuo cha Ufundi ambapo kwa sasa hakuna.
Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amemshukuru Rais Dkt John Pombe Magufuli kwakuwa mpaka sasa Mkoa wa Songwe umepokea shilingi bilioni 251.6 kwa ajili ya miradi na shughuli mbalimbali za maendeleo.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.