Barabara ya Mpemba Isongole iliyopo Wilaya ya Momba na Ileje yenye Urefu wa kilomita 59.1 imekamilika kwa asilimia 98 na wananchi wameanza kuitumia.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig.Jen.Nicodemus Mwangela ameyasema hayo mapema leo alipoenda kukagua maendeleo ya ujenzi wa barabara hiyo iliyowekewa jiwe la msingi Oktoba 2019 na aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt John Pombe Magufuli ambapo aliagiza barabara hiyo ikamilike mapema kwani inaunganisha pia nchi ya Tanzania na Malawi.
Mkuu wa Mkoa amesema ujenzi wa Barabara hiyo inayojengwa kwa kiwango cha lami unaendelea vizuri sehemu iliyobaki ni kukamilisha Daraja linalounganisha Nchi ya Malawi na Tanzania na kipande cha mita 300 kuwekwa lami kilichopo kwenye Daraja hilo.
"Mkandarasi yupo anaendelea na kazi ya sehemu zilizobaki pamoja na kutatua changamoto zinajitokeza, akimaliza kutakuwa na kipindi cha matazamio cha mwaka moja" Brig. Jen. Mwangela.
Ziara ya Mkuu wa Mkoa imefanyika baada ya kuwepo kwa malalamiko ya wananchi kuwa kuna uharibifu unafanyika kwenye Barabara hiyo pamoja na baadhi ya maeneo kujengwa kwa chini ya viwango.
Aidha Mkuu wa Mkoa amewatoa hofu wananchi kuwa watalamu wa TANROAD walio waadilifu wapo kazini wanafuatilia kila hatua inayofanyika na sehemu ambazo zina shida wamezigundua kwa hatua zaidi.
Meneja wa TANROAD Mkoa wa Songwe Eng. Yohana Kasaini amesema kuna baadhi ya maeneo pembezoni mwa Barabara yamepata nyufa ndogo na kazi anayofanya Mkandarasi kwa sasa ni kuziba zile nyufa kwa kutumia lami Ili maji ya mvua yasiendelee kuingia ndani na kuharibu tabaka nyingine na punde mvua zitakapoisha Mkandarasi ameelekezwa kuyakata hayo maeneo na kufanya uchunguzi wa kina na kuyarekebisha vizuri kwa mujibu wa uchunguzi wa Mkandarasi.Mkuu wa Mkoa ameambatana na wajumbe wa Kamati ya Usalama na viongozi wa Wilaya ya Ileje.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.