Maafisa Kilimo na Ugani wametakiwa kupata mafunzo kuhusu namna ya kuongeza uzalishaji bora wa zao la Kahawa kutoka katika kituo cha utafiti wa zao la Kahawa (TaCRI) kilichopo Mbimba Wilayani Mbozi Mkoani Songwe.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Nicodemas E Mwangela ametoa maelekezo hayo mapema jana wakati alipotembelea kituo cha Tacri-Mbimba ili kukagua shughuli za kituo hicho.
Brigedia Jenerali Mwangela amesema atasimamia kuona maafisa Ugani na Kilimo kutoka halmashauri za Mkoa wa Songwe wanapata mafunzo ili tafiti za zao la kahawa zinazofanyika kituoni hapo ziweze kuwanufaisha wakulima wengi wa Kahawa Mkoani hapa.
“Nimeona hakuna kushikamana kati ya Tacri na Halmashauri za Wilaya, tafiti nzuri wanazofanya bado hazijawafikia wananchi wengi hasa wakulima wadogo ambao kama serikali tunatamani wazalishe vizuri, hivyo basi nitasimamia maafisa kilimo waje hapa kujifunza”, amesisitiza.
Ameeleza kuwa zao la kahawa ni la mkakati kwa mkoa wa Songwe ambalo linaweza kuwakomboa wakulima kutoka kwenye umasikini lakini tafiti zinaonyesha kushuka kwa uzalishaji wa zao hilo.
“Taarifa zinaonyesha mwaka 2015 mkoa ulizalisha tani 12 za kahawa, mwaka 2016 uzalishaji ulishuka mpaka kufikia tani 7 na mwaka 2017 tumezalisha tani 8, takwimu hizi inabidi zipande, tuzalishe kahawa nyingi na bora”, ameongeza.
Brigedia Jenerali Mwangela amesema pia atazisimamia halmashauri ili zitenge asilimia 20 ya mapato yanayopatikana kutoka katika kahawa ili fedha hizo zitumike kuboresha uzalishaji wa kahawa katika halmashauri hizo.
Naye Mtafiti kutoka TaCRI Charles Mwingira amesema kituo hicho kinahudumia wakulima 69,935 kutoka mikoa ya Songwe, Mbeya, Rukwa na Katavi na kimeweza kusambaza miche zaidi ya milioni 7.5.
Mwingira amesema kituo hicho pia kimeweza kusajili na kusambaza aina 23 za miche bora ya kahawa huku miche hiyo ikiwa na sifa za kuzalisha zaidi, zina punje kubwa na bora na ia zinakinzana nan a magonjwa.
Ameongeza kuwa changamoto mojawato inayosababisha kushuka kwa uzalishaji wa za la kahawa ni kutokana na kuwa halmashauri hazijawekeza vizuri katika zao la kahawa.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.