Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe imewapongeza viongozi wa Serikali Ngazi ya Mkoa na Halmashauri, Chama na taasisi za Serikali na ofisi ya Mbunge wa Jimbo la Songwe kwa usimamizi na utekelezaji mzuri wa miradi ya maendeleo katika wilaya hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa, Januari 22, 2023 na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Songwe, Ndugu Radwel Mwampashi wakati wa ziara ya Kamati ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Songwe ya kutembelea na kukagua utekelezaji wa baadhi ya miradi ya maendeleo katika Wilaya ya Songwe.
Akitoa majumuisho ya ziara hiyo, Ndugu Mwampashi amesema kuwa miradi waliyoitembelea katika ziara ya sasa imekuwa na mabadiliko makubwa sana.
"Miradi ya safari hii imekuwa na mabadiliko makubwa sana katika Wilaya ya Songwe kwa kweli kwa niaba ya kamati ya siasa nawapa 'big up'. Nawapongeza sana. Hakuna mradi ambao umekuwa na kasoro na siku zote Wilaya ya Songwe imekuwa roal modal ya Mkoa wa Songwe. Hongereni sana" amesema Mwenyekiti huyo wa CCM Mkoa wa Songwe na kuongeza;
"Mimi kwa niaba ya kamati niwapongeze sana viongozi wa Wilaya ya Songwe. Kazi mnayoifanya ni nzuri lakini pia mambo yanayofanyika mazuri kama haya ni juhudi za mheshimiwa Rais wetu ambaye usiku na mchana halali usingizi kuhakikisha wananchi wanapata huduma"
Pia, amewasisitiza viongozi wa Wilaya hiyo kushirikiana na kuombeana ili Mkoa huo uwe namba moja katika kusimamia na kutekeleza Ilani ya CCM pamoja na kujipanga kuelekea kwenye chaguzi zijazo.
kamati ya Siasa, pia iliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Dkt. Francis K. Michael, Katibu Tawala wa Mkoa, Bi. Happiness Seneda, wataalamu kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa, wametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa umeme wa REA katika Kijiji cha Itindi wenye thamani ya Sh359.7 milioni, ujenzi wa Shule mpya ya Sekondari ya Sambila yenye thamani ya Sh583 milioni na Shule mpya ya msingi ya Kikuyuni yenye thamani ya Sh538.5 milioni ya mradi wa BOOST.
Miradi mingine ambayo kamati hiyo imeitembelea na kuikagua ni pamoja na mradi wa barabara ya Chang'ombe-Patamela-Makongolosi wenye thamani ya zaidi ya Sh4 bilioni na mradi wa ujenzi wa barabara ya Shanta Ndogo-Njelenje ambao unatekelezwa kwa Sh584 milioni.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.