KIKAO KAZI NA KUKARIBISHA MRADI WA UMEME JUA
Mkuu wa Mkoa wa Songwe alifungua kikao kazi cha umeme jua ambacho kilihusisha Mwekezaji Baraka Solar, Wataalam wa Sekretariet ya Mkoa, Wakuu wa Wilaya, Wakurugenzi Watendaji na Wenyeviti wa halmashauri wa Wilaya na Mji wa Tunduma katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi tarehe 10 Agosti,2017
Akifungua kikao hicho Mkuu wa Mkoa aliwataka Washiriki kusikiliza kwa umakini maelezo ya mwekezaji kampuni ya Baraka Solar Specialists Ltd inayojishughulisha na usambazaji, uuzaji na ufungaji wa umeme Jua katika huduma za Jamii, hufunga pampu za kuvutia maji kwa kutumia nguvu ya jua ili kurahisisha upatikanaji wa maji vijijini na asilimia 80 ya miradi hufanywa kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya na Miji Tanzania. Aliongeza kuwa Kampuni ya Baraka Solar imekusudia kuwafikia Wananchi ambao wapo mbali na mpango wa Mradi wa Umeme Vijijini wa REA.
Baada ya ufunguzi huo, Mkuu wa Mkoa aliongea na Washiriki akianzia na hatua ya Mkoa kuhamia kwenye matumizi ya TEHAMA ambapo alizitaka kila Halmashauri kufanya mafunzo ya matumizi ya Tablets ya awali wakati wanasubiria mafunzo ya baadaye ambayo yatahusisha mfumo ambao utawezesha Vifaa hivyo kufanya kazi ya kusambaza, kutunza nyaraka kwa njia ya usalama na ufanisi na siyo kufanya kazi nyingine.
Pia alisisitiza kuwa kila Halmashauri kufanya vikao vya Pembejeo mapema kabla ya msimu wa Kilimo kuanza, alisema ni vizuri kujua pembejeo gani zinahitajika katika Halmashauri kwa kuzingatia maeneo ya kijiografia.
Ili kuhakikisha kuwa Mkoa unapata pembejeo zenye viwango vinavyotakiwa Mkuu wa Mkoa aliagiza kuwa vikao hivyo vihusishe wadau wote wa Pembejeo kwa mfano vyama vya Wakulima, Wasambaza pembejeo n.k. aliagiza kuwa wasambazaji watume maombi ya kuonesha nia ya kusambaza pembejeo na kupata nafasi ya kujieleza watakavyoweza kusambaza pembejeo hizo kwa kuzingatia mikataba itakayoandaliwa na Wanasheria wa serikali.
Mkuu wa Mkoa alisema kuwa kwa kutumia njia hiyo itakuwa rahisi kulinda ubora wa pembejeo na kumfikia mtumiaji kwa wakati pia msambazaji wa pembejeo feki atajulikana kwa urahisi na sheria zitachukua mkondo wake.
Vilevile aliagiza kuwa uendeshaji wa vikao vya Pembejeo wa awali uliohusisha mgao wa pembejeo za ruzuku ubadilike na kuwa na mtizamo mpana zaidi kwa kushirisha Maafisa Kilimo, Maendeleo ya Jamii, Biashara ili wakulima na Halmashauri waweze kunufaika na kuziba mianya ya pembejeo feki katika Mkoa wa Songwe.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.