Uongozi wa machifu Mkoani Songwe umeipongeza serikali kwa kutambua na kuruhusu matumizi ya Tiba za Asili kama vile kujifukiza huku ukiahidi kusimamia matumizi sahihi ya tiba hizo hususani katika kupambana na Ugonjwa wa Corona.
Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Songwe Chifu Mbeshena Nzunda ameyasema hayo wakati alipokutana na Mkuu wa Mkoa wa Songwe kujadiliana namna bora ya kutumia njia za tiba za asili kama vile kujifukiza katika kutibu magonjwa ya mfumo wa upumuaji.
Chifu Nzunda amesema njia ya asili ya kujifukiza kwa kutumia miti, majani au mizizi wanaifahamu na imekua ikitoa nafuu kwa wagonjwa wa mafua na kikohozi huku akiwataka waganga wanaotoa tiba ya kufukiza wasitumie maji ya moto sana wala kufukiza muda mrefu kufukiza.
Amesema machifu wamekubaliana kufuata maelekezo ya serikali huku wakiwasimamia waganga wote na endapo watajitokeza watakaoenda kinyume na utaratibu wa serikali watawaripoti katika vyombo vya sheria pia wagonjwa wasijifukize nyumbani bali wawaone waganga wenye leseni ili wapate tiba sahihi.
Mkuu wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela amewataka machifu kutumia uzoefu walio nao wa kufahamu mizizi, miti na majani yanayo weza kutibu magonjwa mbalimbali watoe tiba hizo bila kuweka masharti yasiyo faa kwa wananchi.
Brig. Jen. Mwangela amesema lengo la serikali ni kutaka shughuli ziendelee licha ya uwepo wa ugonjwa wa Corona pia wananchi wawe na afya njema hivyo tiba za asili zinazo weza kutoa nafuu kwa wagonjwa zinaruhusiwa kutumika.
Naye Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe Dkt Hamad Nyembea amesema tiba za asili hususani njia ya kufukia imekuwa ikitumika katika mataifa mbalimbali na imekuwa ikitoa nafuu kwa wagonjwa wenye matatizo katika mfumo wa upumuaji.
Dkt Nyembea amesema njia ya kufukiza sio tiba kwa asilimia 100 bali hutoa usaidizi kwa mgonjwa wa matatizo ya njia ya hewa aweze kupumua vizuri na pia kujifukiza sio kinga ya ugonjwa wa Corona.
Amesema licha ya serikali kuendelea kutoa matibabu ya hospitali kwa magonjwa ya mfumo wa hewa kama mafua na kikohozi pia kuna umuhimu wa kutopuuzia tiba asili ya kujifukiza kwakuwa hutoa unafuu kwa mgonjwa.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.