Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Mhe. Dkt. Francis K. Michael, amefanikiwa kutatua mgogoro wa ardhi uliodumu kwa zaidi ya miaka 19 baina ya kijiji cha Nanyala na kiwanda cha Saruji cha Mbeya. Hatua hii ya kutatua mgogoro huu imesababisha kutoa suluhisho la kihistoria kwa pande zote husika.
Dkt. Francis, aliwaita pande zote za mgogoro wa ardhi, yaani Kiwanda cha Saruji cha Mbeya na Wanakijiji cha Nanyala, na kuwataka kiwanda cha Saruji cha Mbeya kutoa eneo la hekari 62.5 kutoka kwenye ardhi yao ili kuwapatia wachimbaji wadogo wanaotoka katika kijiji cha Nanyala.
Mbali na kutoa eneo hilo kwa wachimbaji lakini pia kiwanda cha saruji mbeya kimekubali ombi la mkuu wa mkoa kutowafukuza wananchi wanaofanya Shughuli za kilimo na ufugaji katika eneo la kiwanda na badalayake wawaache waendelee kufanya shughuri hizo kwa mikataba ya mwaka mmoja mmoja.
Dkt. Francis alitoa hati miliki ya maeneo kwa wanakijiji wa Nanyala na wamiliki wa kiwanda cha Saruji kilicho mpakani mwa mikoa ya Mbeya na Songwe. amedhihirisha uongozi wake wa kipekee katika kutatua migogoro na kuleta maendeleo kwa wananchi wa mkoa huo. Amesisitiza umuhimu wa amani na ushirikiano katika kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.
Akizungumza, Dkt. Francis alisema, "Nimeteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kutatua changamoto za wananchi. Tunaamini kuwa amani ni msingi wa maendeleo, na leo tumeweza kurejesha amani na furaha kwa wananchi wa kijiji cha Nanyala."
Mkuu wa Wilaya ya Mbozi, Mhe. Esther Mahawe, pia amepongeza juhudi za kila mtu aliyejitolea katika mchakato huu wa kutatua mgogoro huo. Amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo na amani kwa kijiji cha Nanyala.
Wananchi wametoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa, Dkt. Francis kwa kazi yake nzuri katika kuwezesha kutatuliwa kwa mgogoro huo wa ardhi, na kwa kuweka msingi wa maendeleo na amani katika eneo la Songwe. Zawadi ya mbuzi ili tolewa na wananchi ikiwa ni ishara ya ukarimu wa wananchi wa eneo hilo na shukrani kwa uongozi wake wa ujasiri na hekima kubwa katika kutatua migogoro kwa amani.
2 Nselewa Mkoani RD, 54180 Mlowo-Mbozi
Anuani ya Posta: P.O.BOX 23 SONGWE
Simu: 025 2580305
Simu ya Kiganjani: 025 2580305
Barua pepe: ras@songwe.go.tz
Hakimiliki©2020 Mkoa wa Songwe.Haki Zote Zimehifadhiwa.